Rayvanny ajibu madai ya kuwa na ugomvi na aliyekuwa mpenzi wake, Paula Kajala

Staa huyo wa Bongo ameshtumiwa kwa kumtupia vijembe mpenzi huyo wake wa zamani.

Muhtasari

•Bosi huyo wa Next Level Music ameweka wazi kuwa amejikita tu kwenye muziki wake na wala hana ubishi na mwanamke yeyote yule kote duniani.

•Rayvanny aliweka wazi kuwa maneno ya wimbo huo hayakumhusu yeyote bali alikuwa akifanya muziki tu.

Rayvanny ajuta kumpenda Paula
Rayvanny ajuta kumpenda Paula
Image: Maktaba

Staa wa Bongo Raymond Shaban Mwakyusa almaarufu Rayvanny amepuuzilia mbali madai ya kuwa na ugomvi na aliyekuwa mpenzi wake Paula Kajala.

Bosi huyo wa Next Level Music ameweka wazi kuwa amejikita tu kwenye muziki wake na wala hana ubishi na mwanamke yeyote yule kote duniani.

Aikuwa akijibu tuhuma za kumshambulia binti huyo wa muigizaji Fridah Kajala Masanja katika wimbo wake mpya wa 'Tusipanganie'.

"Mbona Paula hana habari nawe, wewe kutwa vijembe, vijembe.. fanya muziki," shabiki mmoja alimwambia Rayvanny chini ya video moja ambayo alichapisha kwa ajili ya kutangaza wimbo huo ambao aliomshirikisha Gnako.

Katika wimbo huo, msanii huyo wa zamani wa WCB anasikika kutuma ujumbe kwa mwanamke asiyetaja jina ambaye tayari ameshaachana naye, sababu tosha ya baadhi ya mashabiki kuamini kwamba anamzungumzia Paula.

Rayvanny hata hivyo katika jibu lake aliweka wazi kuwa maneno ya wimbo huo hayakumhusu yeyote bali alikuwa akifanya muziki tu.

"Nyamaza! Ninafanya muziki wangu kwa ajili ya watu wangu, ninatengeneza vibao kwa ajili ya mashabiki wangu na sina vita na mwanamke yeyote duniani. #tusipangiane," alijibu kwa hasira.

Msanii huyo wa zamani wa Diamond Platnumz amekuwa akijisimamia mwenyewe baada ya kugura lebo ya WCB mapema mwaka huu. Rayvanny aliondoka WCB mwezi Julai baada ya kuwa pale kwa miaka sita. Sasa anaangazia lebo yake ya NLM. 

Mwezi uliopita wakati akitumbuiza katika tamasha la Fiesta 2022 mjini Sumbawanga, Tanzania, Rayvanny alithitisha kutengana na Paula. Alikuwa akiimba wimbo wake 'Naogopa' wakati alikiri kuachana na mwanamitindo huyo wa miaka 20.

"Mapenzi yasikuchanganye nakwambia, usije ukapata bila kama Dulla. Mapenzi usije kufananisha,  kama  vile na chakula. Nilinyosha moyo Karula, nikaachana na Paula..." aliimba.

Rayvanny na  Paula waliweka hadharani mahusiano yao mwaka jana mnamo siku ya Valentine's. Hata hivyo kwa sasa wametengana na mwanamuziki huyo mahiri anadaiwa kurudiana na baby mama wake, Fahyma.