Tembo vs Chui: Harmonize azidisha ugomvi wake na Rayvanny

Konde Boy alimshtumu bosi huyo wa Next Level Music kwa kusambaza picha zake chafu.

Muhtasari

•Harmonize aliwatupia vijembe watu kadhaa ambao aliwahi kugongana nao katika siku za hapo nyuma  na Rayvanny hakuachwa nyuma.

•Ni wazi kuwa Harmonize bado anamtupia lawama Rayvanny kwa kuvujisha picha hizo za uchi mitandaoni..

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE, RAYVANNY

Bosi wa Konde Music Worldwide Harmonize amedokeza kuwa bado ana kinyongo na aliyekuwa  mwenzake katika WCB Rayvanny.

Katika wimbo  ‘My Way’ kwenye albamu yake mpya 'Made for Us', , Harmonize aliwatupia vijembe watu kadhaa ambao aliwahi kugongana nao katika siku za hapo nyuma  na Rayvanny hakuachwa nyuma.

Konde Boy alimshtumu bosi huyo wa Next Level Music kwa kusambaza picha zake chafu mapema mwaka jana na kusisitiza kuwa alichangia  kutengana kwake na mpenzi wake Kajala Masanja.

"Si hasira mawazo yalinisonga. Dogo wa Mbeya (Rayvanny)  aliposambaza mkonga,(picha za uchi).  Haters walidhani nitajinyonga. Sasa ni kweli niko na nguvu zaidi," alisema katika sehemu ya wimbo huo.

Staa huyo wa Bongo alidokeza kuwa yeye na Kajala walipendana sana kabla ya kutengana bila kugombana baada ya tukio hilo la aibu.

Rayvanny alikuwa akichumbiana na binti wao Kajala, Paula wakati Harmonize alipoachana na muigizaji huyo Aprili mwaka jana. Wapenzi hao wawili ambao kwa sasa tayari wamerudiana walitengana baada ya Harmonize kudaiwa kujaribu  kumtongoza Paula kwa jumbe tamu na picha za uchi.

Ni wazi kuwa Harmonize bado anamtupia lawama Rayvanny kwa kuvujisha picha hizo za uchi mitandaoni..

Kupitia wimbo huo 'My Way', Harmonize pia  alidai hakuwahi kutaka kugombana na Diamond ila bosi huyo wake wa zamani alianza kumuoenea kijicho. Alibainisha hakuwahi kuwa na shida na watu waliojaribu kumzuia hapo awali

"Hata huyo ndugu yenu mi sikuvitaka vita. Mbona sikugombana na Madam Rita? Ni pressure ya kuhofia nampita. Akiskia nakohoa karoho kanampita," aliimba.

Aidha, staa huyo wa Bongo alibainisha kuwa hayuko kwenye ushindani na mtu yeyote licha ya mara nyingi kushindanishwa na Diamond.

"Siishi kwa matakwa mtu, siwezi mridhisha kila mtu. Eti nisifanye kitu kumuogopa. Huu muziki ni kipaji sishindani na mtu," alisema.

Pia alibainisha kuwa amejikita katika kujaribu bahati yake maishani na anawajali tu watu wake wa karibu.