Samidoh awashukuru wanawake wawili akisherehekea siku yake ya kuzaliwa

Wa kwanza katika kumbukumbu ya sherehe hiyo alikuwa marehemu mama yake

Muhtasari
  • Anapoanza mwaka mpya katika maisha yake, Samidoh alimwomba Mungu amuongoze katika enzi yake mpya kwa kunukuu mstari wa Biblia unaoomba mwongozo na mafundisho
Samidoh
Image: HISANI

Mwanamuziki wa Mugithi Samuel Muchoki almaarufu Samidoh alisherehekea siku yake ya kuzaliwa mnamo Novemba 1, 2022.

Anapoanza mwaka mpya katika maisha yake, Samidoh alimwomba Mungu amuongoze katika enzi yake mpya kwa kunukuu mstari wa Biblia unaoomba mwongozo na mafundisho.

"Zaburi 25:5: Uniongoze katika ukweli wako na unifundishe, kwa maana wewe ndiwe Mungu Mwokozi wangu, na tumaini langu liko kwako mchana kutwa," Samidoh alisema.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 32, ambaye kwa sasa yuko ziarani nchini Marekani, aliendelea na kuwashukuru wanawake wawili ambao alisema wamechangia pakubwa katika kumfanya kuwa mwanamume aliye leo.

Wa kwanza katika kumbukumbu ya sherehe hiyo alikuwa marehemu mama yake ambaye alimwita kwa jina lake, Miriam, akisema alikuza talanta yake katika umri mdogo na kwamba maombi yake yalikuwa yamejibiwa. Pia alimshukuru baba yake ingawa hakuzungumza mengi juu yake.

"Kwa mwanamke aliyenizaa, Miriam, kila siku naona maombi yako yanatimia, asante kwa kunipa uhai na kukilea kipaji changu katika umri mdogo. Baba, asante kutoka ndani ya moyo wangu,” Samidoh alisema.

Mwanamke mwingine aliyemtaja ni mwanasiasa aliyemtaja kama Betty M. ambaye alimtaja kuwa dira yake akisema huwa anampa maelekezo mara nyingi hasa anapojikuta amefika mwisho

"Mama yangu mlezi Seneta Betty M. Mama wewe ni dira yangu kila mara unanipa mwelekeo ninapotoka, niishi maisha marefu," aliongeza.