Fahamu mzozo wa Amber Ray na shirika la ndege la Kenya Airways

Amber Ray alikuwa akipanga kurudi nchini wakati alipofikiwa na habari za mgomo wa marubani.

Muhtasari

•Shirika la KQ lilighairi safari zake nyingi kufuatia mgomo wa marubani. Mgomo huo uliathiri zaidi ya abiria 10,000

•Ingawa Amberay hakupenda wazo hilo, aliweka wazi kuwa hawataki kurejeshewa pesa bali wapewe vocha kwa ajili ya safari ya baadaye.

Amber Ray na mpenzi wake Kennedy Rapudo
Image: INSTAGRAM// AMBERRAY

Mwanasoshalaiti mashuhuri Amber Ray amefichua kuwa yeye na mpenzi wake Kennedy Rapudo walikuwa miongoni mwa waathiriwa wa kughairishwa kwa safari za shirika la ndege la Kenya Airways siku ya Jumamosi.

Wikendi, shirika la KQ lilighairi safari zake nyingi kufuatia mgomo wa marubani. Mgomo huo uliathiri zaidi ya abiria 10,000.

Amber Ray ambaye alikuwa nchini Mauritius kusherehekea siku yake ya kuzaliwa pamoja na mpenziwe alikuwa akipanga kurudi nchini wakati alipofikiwa na habari za mgomo wa marubani ambao uliathiri safari yao.

"Tuliamua tujipange angalau tusiongeze stress nyumbani kwani naamini wengine wengi tayari wanafanya hivyo. Tuliamua kuchukua ndege nyingine kupitia Dubai (sio KQ)," alisema kupitia ukurasa wake wa Instagram.

Mama huyo wa mvulana mmoja amedai kwamba baadaye shirika hilo la ndege lilijitolea kuwarejeshea shilingi 15,000 tu, ambacho ni kiasi cha chini sana kuliko nauli ambayo walilipa ya Ksh340,000.

Ingawa hakupenda wazo hilo, aliweka wazi kuwa hawataki kurejeshewa pesa bali wapewe vocha kwa ajili ya safari ya baadaye.

"Sio haki kuweka watu wamekwama  bila mawasiliano na pia kutuadhibu kwa kufanya mipango mingine ilhali shida iko upande wenu," alisema.

Amber Ray aliadhimisha siku yake ya kuzaliwa Alhamisi wiki iliyopita. Mwanasoshalaiti huyo alisherehekea kutimiza miaka 30.

Mpenzi wake Kennedy Rapudo alichukua fursa kumwandikia ujumbe mtamu wa mahaba na kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa.

"Heri ya kuzaliwa kwa mwenzangu wa roho, mpenzi wangu na rafiki yangu bora. Daima tuone usiku na mchana pamoja! Heri njema kwa siku ya kuzaliwa malkia, " alimwambia kupitia mtandao wa Instagram.

Aliongeza "Mpenzi wangu, sijawahi kuwa na furaha hadi pale ulipokuwa maishani mwangu. Wewe ni mtu ninayemthamini sana. Katika siku yako hii maalum, ninakuombea mema katika maisha yako, upendo, amani na furaha katika maisha yako. Mungu akufunike kwa upendo wake wa kipekee na akumiminie baraka zake tele."