Mejja afichua kwa nini mahusiano yake yamefanikiwa kwa miaka miwili

Mwimbaji huyo aliweka wazi kuwa bado hayuko tayari kumtambulisha mpenziwe hadharani.

Muhtasari

•Mejja amekiri kwamba amekuwa kwenye mahusiano yasiyojulikana kwa kipindi cha takriban miaka miwili iliyopita.

•Mejja alidokeza kuwa mahusiano yake ya sasa yanaendelea vyema na anatumai yataishia kuwa ndoa ya kudumu.

Image: INSTAGRAM// MEJJA

Mwanamuziki wa nyimbo za kisasa Major Nameye Khadija almaarufu Mejja amekiri kwamba amekuwa kwenye mahusiano yasiyojulikana kwa takriban miaka miwili.

Katika mahojiano na Plug TV, msanii huyo mzaliwa wa Nyeri aliweka wazi kuwa bado hayuko tayari kumtambulisha mpenzi wake wa sasa hadharani.

Alisema kuwa amejifunza kutokana na mahusiano yake ya awali ambayo yalifika kikomo baada ya kumtambulisha mpenzi wake.

"Sasa hivi tunaenda kumaliza miaka miwili  bila shida. Tumekuwa naye (mpenziwe) vizuri kwa miaka miwili," alisema.

Mwimbaji huyo pia alibainisha kuwa mpenziwe hajawahi kumshinikiza kumtambulisha kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo anajivunia.

"Nafikiri ukiweka mahusiano kwenye mitandao, kuna maswara mingi tu hutokea. Hakuna haja ya kuwekea," alisema.

Mejja alikiri kwamba yeye si mkamilifu katika masuala ya mahusiano na kubainisha kwamba hawezi kuwa mfano bora kwa watu ambao wako kwenye mahusiano au wanaopanga kujitosa kwenye uhusiano.

Hata hivyo alidokeza kuwa mahusiano yake ya sasa yanaendelea vyema na anatumai yataishia kuwa ndoa ya kudumu.

"Kwa kweli kila mtu ambaye anachumbiana huwa na matumaini kuwa huo ndio mwisho. Lakini huwezi kujua. Tutajua huko mbele. Lakini vile kunaendelea sio mbaya," alisema mwanamuziki huyo.

Mahusiano ya mwisho ya Mejja yaliyojulikana yalikuwa na anayedaiwa kuwa baby mama wake Milly Wairimu. Wawili hao walitengana kwa njia tatanishi na wamekuwa na uhusiano mbaya baada ya hapo.

Kwa muda mrefu, Milly alikuwa akiibua tuhuma mbaya dhidi ya mwanabendi huyo wa zamani wa kundi la Kansoul. Mejja hata hivyo alisalia kimya asijibu tuhuma nyingi za mpenzi huyo wa zamani.

Katika mahojiano na Massawe Japanni miezi michache iliyopita, Mejja alisema sababu ambayo hajawahi kujibu tuhuma hizo ni kwamba ni za uongo.

"Sijawahi kujibu madai hayo. Nimeendelea na maisha na sijali tena alichosema," alisema.

"Sijamfanyia chochote, sitaki iwe mvutano. Naijua amani yangu. Sijaomba msamaha kwa vile sina hatia."

Mejja aliendelea kusema kuwa meneja wake hajawahi kumtaka azungumzie suala hilo lote.

Alieleza kuwa watu wakome kumwita mwanadada huyo baby mamake.

"Nataka nieleze na ijulikane kuwa yeye sio mama wa watoto wangu, mimi ndiye niliyempenda na watoto wake, nina mtoto wangu wa mama ambaye alinizalia watoto wangu na sio yeye. hata kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii." alisema.