(+video) Mwanaume akimbia akiita mamake baada ya kukutana na 'jini' mtaka damu

Mwanaume huyo baada ya kusikia mwanadada huyo akimuitisha damu, alianza kupagawa na kukimbia akiita mamake kumsaidia.

Muhtasari

• Mwanaume huyo alikuwa amechezewa shere na kundi la wanadada mapacha watatu wanaojiita Comrade Triplets.

Wanadada mapacha watatu wa Kenya ambao wanafanya mitikasi kwenye mitandao ya kijamii kuwachezea shere watu na akili zao, safari hii wamerudi na tukio moja ambalo limezua vichekesho pakubwa.

Watatu hao ambao wanajiita Comrade Triplets walichezea akili za kijana mmoja mwenye umri wa makamo walipomfanyia mzaha mmoja wao akiigiza kama kiumbe kinachohusishwa na unyonyaji damu za watu.

Mary Njenga, mmoja wa mapacha watatu ambaye amejizolea umaarufu mkubwa kama mcheshi, aliigiza kwenye mchezo huo, ambao Wakenya wengi waliangua kicheko.

Kanda hiyo iliyochapishwa mtandaoni mnamo Jumatatu, Novemba 7, ilimuonyesha akimkomalia mwanamume katika eneo lenye vichaka. Alipongeza sura yake kabla ya kumtaka amfuate.

Mwanadada huyo alimsalimia kijana huyo aliyeonekana kuchanganyikiwa kwa kusalimiwa na kidosho mrembo. Baadae alipomuuliza kama atampa damu yake, mwanaume yule kwa kuchanganyikiwa zaidi alianza kukimbilia maisha yake akiwa ameamini kabisa amekutana na jinni mnyonya damu.

Kilichowachekesha wengi ni jinsi kijana wa watu alihaha kutafuta njia ya kuondokea katika eneo hilo lililoonekana kuwa la vichaka huku akimwita mamake kuwa anakufa.

“Unakaa poa, kwani unaniogopa? Si tuende hivi, utanipea damu yako?” Mwanadada huyo aliuliza kabla ya kusimu kuporomoka.

Kijana aliachana mbuga huku mwanadada akijaribu kumfuata nyumba mbio, jamaa huyo alipoangalia nyuma na kuona anafuata na ‘jini’ huyu, alipiga kona na kutafuta njia mbadala kwenda ndani ya vichaka.

Watu kadhaa walichekeshwa na kitendo hicho cha kuzua utani kwa kijana asiyekuwa anatarajia huku baadhi wakikosoa kitendo hicho kwa kusema kuwa ni baba ya mtu anayedhalilishwa.

“Ak si poa, jaribu kufikiria kama angekuwa baba yako?” Mr Skwash aliandika.

“Yani kinadharia aliita jina la mama yake😂😂😂😂aki wanaume tulikosea wapi😂😂😂” mwingine alitania.