Daddy Owen azungumzia kumsamehe aliyekuwa mkewe baada ya talaka yao mbaya

Owen na mkewe wa kwanza Farida Wambui walitengana mwishoni mwa mwaka wa 2020.

Muhtasari

•Daddy Owen amedokeza kuwa tayari amemsamehe mke wake wa zamani Farida Wambui kufuatia kutengana kwao takriban miaka miwili iliyopita.

•Pia alikanusha madai kuwa yuko chini ya shinikizo la kutafuta mke na kuweka wazi kuwa kwa sasa hata hatafuti mchumba.

Bi Farida Wambui na Daddy Owen
Image: HISANI

Mwimbaji wa nyimbo za injili Owen Mwatia almaarufu Daddy Owen amedokeza kuwa tayari amemsamehe mke wake wa zamani Farida Wambui kufuatia kutengana kwao takriban miaka miwili iliyopita.

Owen hata hivyo ameweka wazi kuwa tangu wakati huo amesonga mbele na maisha yake na kudokeza kuwa si rahisi kwa wao kurudiana.

"Mimi ni mtu ambaye kitu ikifanyika nakusamehe lakini nasonga mbele. Kusonga nitasonga, lakini kusamehe nitasamehe," alisema katika mahojiano na Plug TV.

Owen na mkewe wa kwanza Farida Wambui walitengana mwishoni mwa mwaka wa 2020 baada ya kuwa pamoja kwa zaidi ya miaka mitatu kutokana na masuala ya kutokuwepo kwa uaminifu katika ndoa

Msanii huyo mkongwe alisema kwa sasa yuko bize na mambo tofauti na hivyo hajapata muda wa kujikita katika kutafuta suluhu ya mzozo wake na Bi Wambui.

Pia alikanusha madai kuwa yuko chini ya shinikizo la kutafuta mke na kuweka wazi kuwa kwa sasa hata hatafuti mchumba.

"Mimi ni mwanaume, siwezi kutangaza eti natafuta mwanamke. Nikitaka mwanamke nitampata. Mimi ni simba, nitaenda niwinde na nimpate nimtakaye," alisema.

Owen alisisitiza kwamba jambo kuu ambalo atakuwa akilizingatia kwa mwanamke atakapokuwa katika pilkapilka za utafutaji ni sifa ya kumcha Mungu.

Pia alibainisha ni sharti atakayekuwa mkewe awe amelelewa kijijini.

Hivi majuzi mwimbaji huyo alivuma mitandaoni baada ya kudai kuwa anatafuta msichana wa kijijini almaarufu 'Kienyeji' wa kuoa.

"Nataka mwanamke kienyeji mweusi kabisa, mcha mungu, wa kijijini kabisa," alisema katika mahojiano na stesheni moja ya  redio ya humu nchini.

Daddy Owen aliweka wazi kuwa hataki msichana wa mjini akidai kuwa wasichana wa mjini mara nyingi huwa wajuaji sana.

Alisema yuko tayari kumfundisha mke wake kutoka kijijini na kumweka sawa asije akachepuka akionja maisha mjini.

"Awe katika miaka ya 20 au 30," alisema.

Kwenye mtandao wa Instagram, Owen alidokeza kuwa baadhi ya wanadada Wakenya tayari wameanza kujipendekeza kwake.

"Nilisema mwanamke mweusi, watu wanakuja inbox na ati melanin.. ukishasema melanini wewe si kienyeji," alisema.