"Hapana, mimi si mtanashati" - Mwanaume amzima mwanadada aliye msalimia

Baadhi walisema mwanaume huyo aliepuka mtego wa kuombwa pesa.

Muhtasari

• Jibu la Odongo liliwazuzua watu baada ya kumjibu mwanadada huyo kwa kukataa katakata kuwa yeye si mtanashati.

profesa Ochieng Odingo
profesa Ochieng Odingo
Image: Facebook

Mtumiaji maarufu wa Facebook anayetambulika kama Profesa Ochieng Odongo amepakia picha ya mazungumzo yake na mmoja wa mashabiki wake, mazungumzo ambayo yalikuwa mafupi kwa kweli ila yenye kichekesho cha aina yake.

Katika mazungumzo hayo, mtu ambaye katika muktadha wenyewe anadhaniwa kuwa mwanadada alikuwa amemwandikia ujumbe wa kumsalimia huku akimtambua kama mtanashati.

Jibu la Odongo liliwazuzua watu baada ya kumjibu mwanadada huyo kwa kukataa katakata kuwa yeye si mtanashati.

Kama hiyo haitoshi, alizidi mbele kumweleza mwanadada huyo kuwa huenda anamwandikia ujumbe mtu tofauti kwani kwa vile anavyojijua yeye hakuwa mtanashati. Alimtaka mwanadada huyo kufanya utafiti wake mzuri huku akimalizia kwamba hapendi kudanganywa kitu ambacho anajua fika kuwa ni uongo yeye si mtanashati.

“Hello mtanashati,” mtu huyo anayedhaniwa kuwa mwanadada aliandika.

“Hapana, mimi si mtanashati. Tafadhali, chukua muda kujua. Pengine unatuma ujumbe kwa mtu asiye sahihi. Ahsante,” jibu katika mazungumzo hayo lilisoma huku akifuatisha picha hiyo ya mazungumzo na utani kuwa yeye huwa hapendi maneno ya uongo mweupe wa aina hiyo.

Mashabiki wake waliachwa katika vicheko vikubwa huku baadhi wakimwambia kwamba alimpiga bonge la kufuli mwanadada huyo ambaye walihisi alikuwa anajenga mandhari mazuri kama hayo ili kuomba msaada wa pesa.

“Omera unajua mwanamke anarejelea nini anapotumia misamiati hiyo. Wanawake hawatupi Kiingereza kikubwa kama HANDSOME ovyo,” Odhiambo Asetto alisema.