"Rudi nyumbani" Diana Marua afichua anachokosa nyumbani mumewe Bahati akiwa Uganda

Rapa huyo alieleza jinsi anavyotamani kula chakula kilichopikwa na mwanamuziki huyo.

Muhtasari

•Bahati aliondoka nchini siku ya Ijumaa kwa ajili ya matayarisho ya Tamasha hilo ambalo lilifanyika Jumamosi usiku.

•Diana alifichua kuwa Bahati alichukua majukumu ya kupika baada ya kuzaliwa kwa binti yao siku kadhaa zilizopita .

Bahati na Diana Marua
Image: INSTAGRAM// BAHATI

Mwimbaji Bahati ametumia muda mwingi wa wikendi  jijini Kampala, Uganda ambako alikuwa amealikwa kutumbuiza katika tamasha la Eddy Kenzo Festival.

Bahati aliondoka nchini siku ya Ijumaa kwa ajili ya matayarisho ya Tamasha hilo ambalo lilifanyika Jumamosi usiku.

"Kampala Uganda, nitatumbuiza kesho usiku kwenye Tamasha la Eddy Kenzo," alisema siku ya Ijumaa.

Mwimbaji huyo alitua Uganda  siku hiyo hiyo na kushiriki kikao kifupi na Waandishi wa Habari kabla ya kuelekea alikopangiwa kulala.

Katika ukurasa wake wa Instagram, Diana Marua alikiri kwamba alimpeza sana mumewe baada ya kuondoka nchini.

Rapa huyo alifichua kuwa Bahati alichukua majukumu ya kupika baada ya kuzaliwa kwa binti yao siku kadhaa zilizopita na kueleza jinsi anavyotamani kula chakula kilichopikwa na mwanamuziki huyo.

"Kwangu, ni kujitolea kwa  Bahati kuandaa vyakula maalum tangu Malkia alipokuja nyumbani.  Apron inasimulia yote. Nimekosa chakula chako, rudi nyumbani," mama huyo wa watoto watatu alisema .

Aliambatanisha ujumbe huo na picha ya Bahati akiwa amevalia vazi la jikoni huku akiwa amemshika binti yao Heaven Bahati

Diana pia alimthibitishia mumewe jinsi anavyomthamini sana.

Siku chache zilizopita, mwanavlogu  huyo mwenye umri wa miaka 33 alimpongeza mumewe kwa majukumu makubwa ambayo amecheza katika familia yao.

"Mume bora na baba bora wa mwaka, nakutawaza mpenzi wangu Bahati. Umenijali kama mke wako na kuwapenda watoto wako kupita kiasi kila siku," Diana alimwambia Bahati huku akitambua juhudi zake kufanikisha siku  yakuadhimisha kuzaliwa kwake.

Diana alimkaribisha mtoto wake, Malkia Bahati, siku tano kabla ya siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwake. Alitimiza miaka 33.

Mnamo siku ya kuadhimisha kuzaliwa kwa Diana, Bahati alisema rapa huyo ndiye mwanamke aliyeyapa maisha yake maana.