Rapa Noti Flow asimulia ajali iliyomwacha mpenziwe King Alami bila mkono wa kulia

Mguu wa kulia wa Alami pia ulivunjika na goti lake la kushoto likateguka.

Muhtasari

•King Alami alipoteza mkono wake wa kulia katika eneo la tukio wakati alipopata ajali, mpenzi wake Noti Flow amefichua.

•Noti Flow alidai  hafahamu yaliyotokea wakati wa ajali hiyo ambayo ilimwacha Alami na majeraha mabaya. 

King Alami na Noti Flow
Image: INSTAGRAM// NOTI FLOW

Armaan Bux almaarufu King Alami alipoteza mkono wake wa kulia katika eneo la tukio wakati alipopata ajali, mpenzi wake Noti Flow amefichua.

Katika kipindi cha Maswali na Majibu ambacho alishirikisha mashabiki wake kwenye Instagram siku ya Jumatatu, Noti Flow alieleza kuwa mpenzi wake alijeruhiwa vibaya baada ya kuanguka kutoka ghorofa ya saba.

"Je, mkono wake umekatwa, nauliza tu usikasirike," mtumizi mmoja wa Instagram alimuuliza.

Noti Flow ambaye alionekana kuzidiwa na hisia alijibu, "Ndiyo😭, mkono wake wa kulia."

Aliongeza "Aliupoteza katika eneo la ajali😭"

Kando na kupoteza mkono, rapa huyo alifichua kuwa mguu wa kulia wa Alami ulivunjika na goti lake la kushoto likateguka.

King Alami alilazimika kufanyiwa upasuaji mara nyingi katika juhudi za kurekebisha hali yake na npenziwe ameeleza matumaini yake kuwa mwishowe ataweza kutembea tena.

"Madkatari wanasema ataruhusiwa kuenda nyumbani hivi karibuni. Labda masiku. Anapona haraka sana Alhamdulillah... madkatari wanasema ataweza kutembea tena katika siku za usoni. Tuombe iwe hivi karibuni," alisema Noti Flow.

Rapa huyo hata hivyo aliweka wazi kwamba hafahamu yaliyotokea wakati wa ajali hiyo ambayo ilimwacha Alami na majeraha mabaya.

Aliweka wazi kwamba hakuwa pamoja na mpenzi huyo wake mnamo siku ya ajali. Kufuatia hayo,  ametoa wito kwa watu kumruhusu King  Alami apone kwanza ili aweze kueleza ukweli kuhusu kilichotokea.

"Tusimuweke chini ya shinikizo wakati atakaporudi kwenye mitandao ya kijamii. Sio kila mtu huwa tayari kuzungumza kuhusu tukio la kutisha na la kubadilisha maisha kama hili," rapa huyo aliomba.

Kumekuwa na tetesi kuwa King Alami aliruka kutokaorofa ya saba ya jengo kufuatia kutengana kwake na Noti Flow. Wawili hao walikuwa wamekuwa wametengana siku chache kabla ya ajali hiyo kutokea.

"Ninalaumiwa na watu wengine nami nashangaa tu! Asanteni  kwa kunifanya nijisikie mwenye hatia na mbaya zaidi ya jinsi ninavyojiskia tayari. Unapoachana na mtu huwa hutarajii mambo kama haya yatokee lakini sawa. Propaganda na kunyoosheana vidole vya lawama hazihitajiki kwa sasa, tushughulikie tu hali iliyopo. Tena, sijui nini kilitokea," Noti Flow alisema kuhusu tetesi za kuhusika katika tukio hilo.

Rapa huyo pia alifichua kwamba aliyekuwa pamoja na Alami wakati wa tukio hilo alikamatwa na kuachiliwa kwa dhamana huku kesi hiyo bado ikiwa mikononi mwa polisi. Alisema mpenziwe atatoa taarifa baada ya kupata afueni.