Mimi mwanaume akiniambia ananipenda hiyo ni vita - Mwanaume wa Meru asema

Mwanaume huyo alisema kuwa huko Meru mwanaume kumtamkia mwenzake kuwa anampenda ni mwiko na kinyume na tamaduni.

Muhtasari

• Wacha tu Yesu atupende atuambie anatupenda - mwanaume huyo wa Meru alisema.

Mwanaume apinga dhana ya mwanaume kuambia mwenzake anampenda
Mwanaume apinga dhana ya mwanaume kuambia mwenzake anampenda
Image: NTV Screengrab

Jumamosi dunia nzima ilikuwa inasherehekea siku ya kuwathamini wanaume. Runinga ya NTV ilitembea mitaani kutaka kujua hisia za baadhi ya wanaume jinsi watafikiria mwanaume mwenzao akimtamkia kuwa anampenda kama njia moja ya kumsherehekea katika siku hiyo.

Kinyume na wanawake ambao aghalabu wanatumia maneno ya mapenzi kuwapongeza wanawake wenzao, wanaume wengi walionekana kupinga vikali dhana hiyo na kusema kwamba mwanaume kumtamkia mwanaume mwingine kuwa anampenda ni mwiko na kinyume na tamaduni za Kiafrika.

Wachache walikubali kuwa wanatumia maneno hayo ya kimapenzi kuwahongera marafiki zao wa kiume ila wengine pia wakasema iwapo itabidi watumie maneno hayo basi kutakuwepo na mipaka – wakisema kuwa mtu wa kiume ambaye anaweza kumtamkia kuwa anampenda labda ni mtoto wake wa kiume na babake tu basi!

“Mimi siwezi, lakini kuna njia za kujieleza kwa wanaume wenzetu kama wanaume, kwa mfano ‘uko sawa kaka’ hivo tu,” mmoja alisema.

“Mimi nitamwambia tu ndugu yangu, mtoto wangu na babangu, lakini wengine siwezi kabisa, hiyo itakuwa tunachoma kabisa,” Mwanahabari alisema.

Mwanaume mmoja kutoka kaunti ya Meru aligeuka gumzo baada ya kutoa maelezo ya kina ni kwa nini hawezi kabisa kumtamkia mwanaume mwenzake kuwa anampenda – hata baba yake hawezi.

“Vitu vingine acha vibaki tu kwa roho, wacha kama unapenda mwanaume, san asana babako na hata kama unampenda hufai kumwambia hivo, mwambie unamkubali. Wacha tu Yesu atupende atuambie anatupenda. Lakini ikija ni mwanaume kwa mwanaume mwingine hiyo hapana, weka hadithi kama hiyo mbali na masikio yetu. Sisi tunajua tunapendana lakini hatufai kuambiana hivo, ni kinyume na tamaduni haswa hapa kaunti ya Meru. Mimi ukiniambia unanipenda kwanza ni vita kwa sababu unatoa wapi nguvu na ujasiri wa kumwambia mwanaume unampenda?” mwanaume huyo aliuliza.

Alisema kwamba yeye hata mwanaume akimwandikia kimakosa ujumbe kuwa anampenda, anaifuta mara moja na kumtafuta juu chini ili kupambana naye kiume kwa vita vikali.