Mwizi Sacco: Unaweza wekeza pesa zako hapa?

Bango hilo lililoonekana Uganda limezua mjadala mkali kwa wapenzi wa Kiswahili kutokana na ukinzani uliopo katika maana na maudhui yake.

Muhtasari

• “Waganda wanachukia Kiswahili sana ndio maana hata jina Mwizi kwao ni la ustaarabu,” mwanasheria Collins Wanderi alisema.

Bango tatanishi la sacco inayoitwa Mwizi
Bango tatanishi la sacco inayoitwa Mwizi
Image: Instagram//Billy Miya

Bango moja nchini Uganda likitangaza biashara ya uwekezaji, yaani Sacco limezua mjadala mkali mitandaoni nchini Kenya haswa kutokana na jina la kampuni hiyo.

Bango hilo lilikuwa likitoa maelezo ya upande wa biashara hiyo ya Sacco na jina lake lilikuwa ni ‘Mwizi Sacco’ jina ambali kwa Kiswahili lina maana ya wizi.

Jina hili wengi walilichukulia kama kinaya kwani hakuan vile unaweza fungua sacco ya kuwekeza pesa za watu na unaiita jina linalohusishwa na vitendo vya kuiba.

Mtangazaji Billy Miya alipakia picha hii na kuuliza swali moja ambalo linagonga kwa mara moja katika kichwa cha yule aliyeiona;

“Unaweza wekeza pesa zako hapa?” aliuliza.

Wakenya walitoa maoni yao huku wengine wakisema kuwa Uganda jina la Mwizi linamaanisha kitu tofauti na katika lugha ya Kiswahili ambayo imekumbatiwa na watu wengi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Waganda wanachukia Kiswahili sana ndio maana hata jina Mwizi kwao ni la ustaarabu,” mwanasheria Collins Wanderi alisema.

“Lakini ni nani aliyewadanganya hadi kufikia hivi? Lazima uwe Mkenya mwenye nia ya kufanya biashara ya ulaghai,” mwingine alisema.

Wengine walionekana kutetea jina hilo kwa kusema kwamba kwao lina maana tofauti kabisa, wakitoa mfano wa baadhi ya majina kutoka nchini Japan.

Itakumbukwa miezi kadhaa mwaka huu gwiji wa mpira wa vikapu kutoka Japan, Naom Osaka alitangaza kuanzisha kampuni yake ya habari ambayo jina lake katika lugha ya Kiswahili lilikuwa na maana tofauti, jambo ambalo lilizua gumzo kali kwa watu waliokuwa wanaelewa Kiswahili.