Jux kuwakutanisha mahasidi wa muda mrefu Diamond Platnumz na Harmonize

Zaidi ya wasanii 20 wakubwa wamealikwa kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa albamu ya Jux.

Muhtasari

•"Naomba mje wote, karibuni nyote, nawapenda sana," Jux aliwaomba mashabiki wake katika video ya matangazo.

• Diamond  na Harmonize ni miongoni mwa wanamuziki tajika ambao Jux amealika katika hafla hiyo.

Image: INSTAGRAM// JUMA JUX

Staa wa Bongo Juma Jux ameandaa hafla ya uzinduzi wa albamu yake mpya Kings of Hearts ambayo itakafanyika siku ya Jumatano.

Hafla hiyo imeratibiwa kufanyika katika ukumbi wa The Super Dome Masaki, jijini Dar es Salaam ambapo Jux anatarajiwa kutumbuiza mashabiki na wageni waalikwa  kwa nyimbo zote kumi na sita zilizo kwenye albamu hiyo yake

"Naomba mje wote, karibuni nyote, nawapenda sana," Jux aliwaomba mashabiki wake katika video ya matangazo.

Mwanamuziki huyo aliwaelekeza mashabiki wake katika vituo kumi ambako wanaweza kununua tiketi za kuhudhuria hafla hiyo.

Zaidi ya wasanii ishirini wakubwa wa Tanzania wamealikwa kuhudhuria hafla hiyo ya usiku wa Jumatano. 

Bosi wa WCB Diamond Platnumz na aliyekuwa msanii wake Harmonize ambao wamekuwa wakizozana kwa kipindi kirefu ni miongoni mwa wanamuziki tajika ambao Jux amealika katika hafla hiyo.

"Ndugu yangu tangu siku ya kwanza @diamondplatnumz atakuepo The Super Dome kesho kwenye uzinduzi wa Kings of Heart. Kujeni tusherehekee muziki na utamaduni. Kujeni tuimbeni pamoja, tucheze densi pamoja na tusherekee upendo pamoja," Juma Jux aliandika chini ya bango la kumualika Diamond.

Mpenzi huyo wa zamani wa Vanessa Mdee alichapisha bango sawa la mwaliko wa Harmonize.

"Kakangu kutoka Konde Gang @harmonize_tz atakuepo kesho The Super Dome kwenye Kings of Heart Album," aliandika.

Wanamuziki wengine ambao mmiliki huyo wa duka la African Boy aliwaalika kwenye uzinduzi wa albamu yake ni pamoja na Rayvanny, Ommy Dimpoz, Hamisa Mobetto, Lil Ommy, AY, Abby Chamz na Saraphina.

Muigizaji Irene Uwoya, Lulu Diva, Shilole, B Dozen, Fred Vunjabei, Majizzo, Young Lunya, Tessie na Gigy Money pia wamealikwa.

Nyimbo katika albamu Kings of Hearts ni pamoja na Lucky Now, Sina Neno, Sing For You, I Love You, Mapepe, My Mind, Simuachi, Nidhibiti, Kitanda, Only You I See, Found Love, Number One,  Wena, Show Dem, Sumu , Nice (Kiss).