Pritty Vishy afunguka kuhusu kurudiana na Stivo Simple Boy

Vishy aliweka wazi kuwa hana nia ya kurudiana na mpenziwe yeyote wa zamani.

Muhtasari

• Pritty Vishy amefutilia mbali uwezekano wa yeye kurudiana na mpenzi wake wa zamani, mwanamuziki Stivo Simple Boy. 

•Vishy sasa ameweka wazi kwamba yeye ndiye aliyekatiza mahusiano yao ya muda mrefu wala sio Stivo.

Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Stivo Simple Boy na aliyekuwa mpenzi wake Pritty Vishy
Image: SCREENGRAB// MUNGAI EVE

Aliyekuwa mpenzi wa Stivo Simple Boy, Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy amefutilia mbali uwezekano wa yeye kurudiana na mwimbaji huyo kutoka Kibra.

Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha Maswali na Majibu kwenye mtandao wa Instagram siku ya Jumatano,  mtumbuizaji huyo mwenye umri wa miaka 21 aliweka wazi kuwa hana nia ya kurudiana na mpenzi wake yeyote wa zamani.

Vishy alisema tayari amesonga mbele na maisha yake baada ya kutengana na Simple Boy na akabainisha kuwa hayupo tayari kumpa msanii huyo nafasi nyingine.

"Unaweza kumpa Stivo nafasi nyingine?" shabiki mmoja aliuliza.

Vishy alijibu, "Hapanaaa, nimesonga mbele siwezi adi."

Kipusa huyo aliwakosoa wanamitandao wengi waliomshinikiza arudiane na mwimbaji huyo wa kibao 'Vijana Tuache Mihadarati' ili kumsaidia kuendelea kujenga jina lake huku akisema kuwa  yeye ni mkubwa kutosha kujitunza.

"Si ninyi ni wale wale walioniita majina na kusema namtumia? Kwa hiyo wakati mnamuona ako kwenye shida ndo mnaona nilikuwa wa maana?

Heeeh, yeye ni mwanaume bana mtu ako na miaka 33 anasaidiwa na mtoto wa miaka 21 aje.. muache mchezo," alisema.

Pritty Vishy na Simple Boy walitengana mapema mwaka uliopita, miezi michache tu baada ya mahusiano yao kufichuka hadharani. Mahusiano ya wawili hao yalikuja kujulikana na Wakenya  baada ya Vishy kuchapisha video kwenye mitandao ya kijamii iliyoonyesha wakifurahia muda pamoja chumbani mwake.

Mtumbuizaji huyo sasa ameweka wazi kwamba yeye ndiye aliyekatiza mahusiano yao ya muda mrefu wala sio Stivo.

"Hakuvunja moyo wangu mpendwa kwa sababu sio yeye aliyemaliza mambo, mimi ndiye," alijibu shabiki aliyehoji ikiwa anamlaumu mwimbaji huyo.

Vishy aliweka wazi kuwa nguvu aliyosalia nayo kwa sasa ni ya kujijenga mwenyewe wala sio ya kujenga wengine jinsi alivyomsaidia Stivo. Aidha, alidai kwamba mwimbaji huyo kutoka Kibra hakuonyesha shukrani kwa jinsi alivyomsaidia.

Pia alidokeza kwamba tayari kuna mtu mwingine maalum katika maisha yake kwa sasa ambaye hakufichua utambulisho wake.