"Bajeti ya Uber!" Kajala amnunulia bintiye Paula gari jipya baada ya kumtema Harmonize

Paula Kajala ni mmiliki mpya wa gari jipya la kibinafsi aina ya CROWN.

Muhtasari

•Paula alipokea gari hilo la rangi nyeupe kama zawadi kutoka kwa mama yake muigizaji Kajala Masanja siku ya Jumamosi.

•Mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize pia alizidiwa na hisia baada ya kuona jinsi binti yake alivyoipenda zawadi aliyomnunulia.

Paula Kajala na mama yake Kajala Masanja.
Image: INSTAGRAM// KAJALA MASANJA

Mwanamitindo na mjasiriamali wa mavazi wa Tanzania Paula Paul Kajala ni mmiliki mpya wa gari jipya la kibinafsi aina ya CROWN.

Kipusa huyo mwenye umri wa miaka 20 alipokea gari hilo la rangi nyeupe kama zawadi kutoka kwa mama yake muigizaji Kajala Masanja siku ya Jumamosi na kufichua habari hizo njema kwenye ukurasa wake wa Instagram.

"Asante mama, nakupenda sana," Paula alimwambia mzazi huyo wake baada ya kuona na kupokea zawadi hiyo maalum.

Katika video iliyochapishwa na Paula kwenye Instagram, Kajala anaonekana akimbeba bintiye wa pekee kwa gari lake hadi eneo ambalo gari hilo mpya lilikuwa limeegeshwa. Muigizaji huyo alikusudia kumsurprise Paula.

Baada ya kufika eneo ambalo gari hilo lilikuwa, wawili hao walipokewa na watu wengine kadhaa waliokuwa wamekusanyika pale. Punde baada ya kufumbua macho na kuona kile ambacho mama yake alikuwa amemfanyia, Paula alishindwa kuzuia furaha yake kubwa na hivyo kuangua kilio cha furaha.

"Usilie, bajeti ya Uber," Kajala anasikika akimwambia bintiye.

Mpenzi huyo wa zamani wa Harmonize pia alizidiwa na hisia baada ya kuona jinsi binti yake alivyoipenda zawadi aliyomnunulia.

Haya yanajiri takriban miezi sita tu baada ya muigizaji Kajala kuweka bango kubwa lenye picha ya binti yake kando ya barabara moja kuu nchini Tanzania mnamo siku ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa ya 20.

Kajala ambaye wakati huo alikuwa nchini Qatar kwa ziara ya kikazi alifanya bango lenye picha ya bintiye na maandishi  ya kumsherehekea kuwekwa kando ya barabara iliyo katika eneo la Posta nchini hiyo jirani.

"Kheri za siku ya kuzaliwa Paula. Mama anakupenda," Maandishi ya bango hilo yalisoma.

Bila shaka, Kajala na bintiye wana uhusiano mkubwa sana. Wawili hao wanaishi, si tu kama mama na binti, bali pia kama marafiki wakubwa.

Mara nyingi Paula na mama yake huwa wanasaidiana, kushauriana na kuteteana katika masuala mbalimbali ya kimaisha.