Kijana achoma nyumba ya marehemu kakake baada ya mkewe kukataa kuwa mke wake

Kijana huyo aliruhusiwa kuishi na shemeji yake mjane mpaka tambiko la baada ya kifo limefanyika.

Muhtasari

• Alipewa kibali na wazee kukaa na mke wa marehemu ndugu yake kwa muda mpaka shughuli ya tambiko la baada ya kifo limekamilika.

• Baada ya kukamilika, kijana aliyeonja utamu wa Yesu alikataa kuondoka katika nyumba hiyo.

• Aliposhrutishwa, aliona suluhu pekee ni kuitia moto nyumba ya shemeji yake mjane.

moto
moto
Image: Maktaba

Katika mila na tamaduni za kitambo barani Afrika, mwanaume alikuwa anaruhusiwa kurithi mke wa ndugu yake ikitokea ndugu yake huyo amefariki.

Kadri muda ulivyozidi kusonga na usasa kubisha hodi, mila hizo katika sehemu nyingi zimeonekana kuachwa hata ingawa kuna baadhi ya jamii ambazo zinaendeleza mila hizo kinyemela.

Nchini Zambia, kijana mmoja mweney umri wa miaka 22 alisababisha madhara makubwa baada ya kuchoma nyumba ya shemeji yake (mke wa marehemu ndugu yake) alipoambiwa amuache.

Kulingana na jarida la Mwebantu nchini humo, kijana huyo kwa jina Titon Kapanshya alianza kuishi na mke wa ndugu yake kufuatia kifo cha ndugu huyo yake.

Baada ya mazishi kukamilika na matambiko ya kitamaduni kufanywa, wazee wa ukoo walimtaka Kapanshya kuondoka katika nyumba ya shemeji yake mjane lakini kijana wa watu baada ya kuonja utamu wa Yesu kama Rose Muhando, aliamua kukaidi amri ya wazee.

Si tu kukaidi bali pia alizusha mikwara kwa wazee hao kuwa endapo wangeendelea kumwekea shinikizo la kuondoka katika nyumba ya marehemu ndugu yake, basi angefanya moja kati ya kuondoa uhai wake au kuchoma nyumba hiyo moto.

Na kweli kama hakuwa anazungumza mzaha, alizidiwa na shinikizo la kuondoka na akaamua kutia nyumba ya mjane shemeji yake moto.

Mwanaume huyo alitiwa nguvuni na kufikishwa katika kituo cha polisi akisubiri kufunguliwa mashtaka ya uharibifu wa mali ya mjane.

“Familia ilimchagua Bw Kapanshya kwenda kumsafisha mjane mnamo Desemba 10,2022 na wakaanza kukaa pamoja na mke wa marehemu kaka. Baada ya siku kadhaa aliambiwa atoke nje ya nyumba hiyo kwa vile alikuwa amemsafisha lakini aligoma kufanya hivyo kwa kuwa alitaka kuendelea kukaa na mke wa marehemu kaka yake kama mke wake wa pekee hata hivyo mjane hakumtaka tena kwa vile tambiko lilikuwa limekwisha. Kwa hiyo akamtoa nje ya nyumba yake. Bw Kapanshya alikasirishwa na kumtishia kwamba angejiua au kuchoma nyumba,” Kamanda wa polisi alinukuliwa na Mwebantu.