"Ulitaka nijiuwe na bado nipo!" Harmonize amkashifu Rayvanny kwa kuanika uchi wake

Harmonize alimkumbusha Rayvanny mzozo wao uliosambaratisha mahusiano yake na Kajala.

Muhtasari

•Mastaa wa Bongo Harmonize na Rayvanny walikabiliana moja kwa moja kwa vita ya maneno kwenye mtandao wa Instagram.

•Rayvanny  alijigamba kuwa yeye ni bora zaidi kuliko Konde Boy katika masuala ya ubunifu na utayarishaji wa muziki.

•Harmonize alisisitiza kuwa Rayvanny bado yuko chini ya usimamizi wa WCB na hivyo akamwambia hayuko kiwango sawa na yeye.

Image: INSTAGRAM// HARMONIZE, RAYVANNY

Siku ya Jumatatu, mastaa wa Bongo Harmonize na Rayvanny walikabiliana moja kwa moja kwa vita ya maneno kwenye mtandao wa Instagram.

Makabiliano makali ambayo wasanii hao walipeleka kwenye Instastories zao yalianza pale Harmonize alipowashauri wasanii wa Bongo kuacha kutengeneza nyimbo za kuhamasisha pombe na Rayvanny akaamua kujibu.

"Wasanii punguzeni nyimbo za Pombe!! Msidhani hii nchi kila mtu ni mlevi😂 Hata tunaokunywanga Juma 3 Hatunywi tukisikia nyimbo za Pome kama unatonesha Kidonda!! Hasa Hasa January Hii," Harmonize aliandika.

Katika jibu lake, Rayvanny alibainisha kuwa mwenzake huyo wa zamani katika WCB hajawahi kutoa wimbo wa pombe uliovuma.

Rayvanny alibainisha kuwa yeye alihusika katika wimbo mkubwa wa Pombe wakati Harmonize akiwa bado anahangaika.

"Mandakiwe, Huo sio wimbo wako. Shukuru wa Kusini," alisema.

Vita hivyo vilichukua mkondo mwingine wakati wawili hao walianza kuingiliana katika maelezo ya kibinafsi na kujilinganisha katika suala la mafanikio.

"Ulilipa Wasafi 600M ukalia kwenye mitandao ya kijamii,kama hujui nililipa Wasafi bilioni 1.3 ukihisi naongeza sifuri fatilia au nenda BASATA ukaulize na umeona nimeongea wapi? pesa sio kitu kwangu kikubwa ni heshima ndio kitu ninachokithamini ukiona siku nimeongea ujue nimekosewaheshima kupita kiasi,"Aliongea Rayvanny.

Bosi huyo wa lebo Next Level Music alimkumbusha mwenzake huyo wa Konde Music Worldwide kuwa bila bosi wao wa zamani Diamond Platnumz hangekuwa ameweza kufika kilele ambacho amefanikiwa kufika kwa sasa.

Pia alijigamba kuwa yeye ni bora zaidi kuliko Konde Boy katika masuala ya ubunifu na utayarishaji wa muziki.

Wakati vita hivyo vya mtandaoni vikiendelea, Harmonize alimuuliza mwimbaji huyo mwenzake kwanini anamchukia sana. Bosi huyo wa Kondegang alichukua fursa hiyo kumkumbusha Rayvanny kuhusu mzozo wao wa hapo awali ambao ulisambaratisha mahusiano yake na Kajala mwaka wa 2021.

"Ulifanya kila mtu aone sehemu yangu ya siri, ulitaka nijiuwe na bado niko hapa. Usinichukie wenda Mungu ananiweka kwaajili yako uendelee kuwa inspired . Kuja kwa nyumba yangu nitakuonyesha jinsi ya kutengeneza pesa uweze kulipa label (WCB) ili uweze kutoka kabisa," Aliandika Harmonize.

Konde Boy alisisitiza kuwa Rayvanny bado yuko chini ya usimamizi wa WCB na hivyo akamwambia hayuko kiwango sawa na yeye.