(VIDEO)Vipusa wazoa kioja harusini baada ya kulimana makonde kwa ajili ya chakula

Mwathiriwa alipigwa kichwani mwake na kioo hicho, na kuwafanya waliokuwa karibu naye kujificha.

Muhtasari
  • Video za mzozo huo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zikiwaonyesha wageni wakirushiana vyakula, vyombo na chupa

Sherehe ya kifahari ya harusi ya kitamaduni iliyofanyika hivi majuzi katika eneo bunge la Mvita mjini Mombasa iligeuka kuwa ya mtafaruku baada ya vita kuzuka kati ya baadhi ya wageni.

Video za mzozo huo zilisambazwa kwenye mitandao ya kijamii, zikiwaonyesha wageni wakirushiana vyakula, vyombo na chupa.

Video moja, haswa, inaonyesha mwanamke akimlenga mwanamke mwingine na kioo.

Mwathiriwa alipigwa kichwani mwake na kioo hicho, na kuwafanya waliokuwa karibu naye kujificha.

Katika video hizo, mwanamke huyo aliyejeruhiwa anaweza kuonekana akikimbia kutafuta usalama huku damu ikimwagika usoni mwake na kwenye mavazi yake.

Tukio hilo pia limezua mjadala kwenye mitandao ya kijamii, huku wengi wakikisia sababu ya vita hivyo.

Kulingana na duru za habari ni kuwa wanawake hao walikuwa wanazozania chakula, ambacho kilisababisha vita hivyo.

Wengine walisema kuwa tukio hilo ni kiashiria cha kualika watu wachache wa karibu kwenye harusi, ili kupunguza uwezekano wa kukutana kwa aibu.

Sehemu ya wanamtandao pia waliwahurumia wanandoa waliokuwa wamepanga harusi hiyo.