Aliyekuwa mpenzi wa Stivo Simple Boy, Pritty Vishy ajibu kuhusu kuwa shoga

Vishy alijibu, "Kama ndiyo au hapana siwezi kujieleza rafiki yangu."

Muhtasari

•Mfuasi wake mmoja alimtaka afafanue kuhusu madai ya usagaji ambayo yamewahi kumkabili hapo awali.

•Vishy sasa amefichua kwamba moja ya hofu yake kubwa sasa ni kupenda tena.

Pritty Vishy amejibu kuhusu kuwa shoga
Pritty Vishy amejibu kuhusu kuwa shoga
Image: INSTAGRAM// PRITTY VISHY

Aliyekuwa mpenzi wa mwanamuziki Stivo Simple Boy, Purity Vishenwa almaarufu Pritty Vishy aliwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha Maswali na Majibu kwenye Instagram siku ya Ijumaa jioni.

Katika kipindi hicho, wanamitandao walichukua fursa kumhoji mtumbuizaji huyo juu ya masuala mbalimbali yanayohusu maisha yake kuanzia masuala ya kibinafsi, mahusiano na mafanikio yake.

Mfuasi wake mmoja alimtaka afafanue kuhusu madai ya usagaji ambayo yamewahi kumkabili hapo awali.

"Je, Wewe ni msagaji? Kama ndiyo au hapana toa maelezo kwanini?" Shabiki alihoji.

Vishy alijibu, "Kama ndiyo au hapana siwezi kujieleza rafiki yangu."

Madai kwamba mrembo huyo mwenye umri wa miaka 21 huenda kwa kiasi fulani ni msagaji yalichimbuka mwishoni mwa mwaka jana baada ya kuonekana akijivinjari na kubusu na rafiki yake mwanamke.

Mwezi Desemba mwaka jana Pritty Vishy alizua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuonekana akijivinjari na TikToker Becky Akinyi kwa njia ya kimahaba. Wawili hao walifurahiya muda pamoja kwenye eneo la burudani na kuchapisha baadhi ya matukio kwenye kurasa zao za Instagram.

Marafiki hao pia walishirikisha mashabiki wao katika kipindi cha moja kwa moja ambapo walionekana wakibusu mara kadhaa kwenye midomo huku wakibugia vinywaji. Wawili hao walionekana kuwa kwenye klabu.

Wanamitandao walitoa maoni chini ya video ya wawili hao waliibua maswali mengi wakitaka kufahamu uhalisi wa uhasiano wao.

Vishy pia ni miongoni mwa watu ambao walihudhuria mazishi ya mwanaharakati wa haki za wapenzi wa jinsia moja Edwin Chiloba siku chache zilizopita. Chiloba alidaiwa kuuwa na mpenzi wake Jackton Odhiambo.

Hapo awali hata hivyo, Vishy aliwahi kuwa kwenye mahusiano ya kimapenzi na mwanamuziki kutoka Kibra Stivo Simple Boy. Hata hivyo aliwahi kufichua kwamba hakuwahi kushiriki mapenzi na mwimbaji huyo.

Wawili hao walitengana mapema mwaka jana baada ya Vishy kumshtumu mwanamuziki huyo kwa kutokuwa mwaminifu.

Vishy sasa amefichua kwamba moja ya hofu yake kubwa sasa ni kupenda tena.