Nameless ajibu baada ya kuagizwa afanye kipimo cha DNA kwa bintiye mchanga

Mwimbaji huyo alionyesha picha ya Shiru akiwa amelala vizuri kwenye miguu yake mirefu.

Muhtasari

•Shabiki mmoja alitilia shaka mapenzi yake kwa msichana huyo wa miezi mitatu kutokana na jinsi alivyomshikilia na hata kumtaka amfanyie vipimo vya DNA.

•Nameless alicheka maoni hayo na kudokeza kuwa huenda mwanamitandao huyo anasumbuliwa na hali inayohitaji matibabu maalum.

Image: FACEBOOK// NAMELESS

Mwimbaji mkongwe David Mathenge almaarufu Nameless bila shaka anajivunia uzazi na kufurahia majukumu ya baba wa mtoto mdogo.

Nameless amekuwa akichapisha picha zake akiwa na binti yake mdogo, Shiru tangu mkewe Wahu Kagwi alipojifungua Oktoba mwaka jana.

Katika chapisho lake la hivi majuzi kwenye Facebook, alionyesha picha ya Shiru akiwa amelala vizuri kwenye miguu yake mirefu.

"Tunaita huu mtindo wa kukaa wa"the princessthrone", unaotumika kuwaweka mtoto na baba salama, salama na starehe! Naweka hapa kwa nafasi zingine za kiubunifu za kubeba na kukaa watoto," alisema kwenye posti hiyo.

Mamia ya mashabiki wake walitoa maoni kuhusu chapisho hilo, wengine wakifanya mzaha kuhusu jinsi alivyomshika bintiye, wengine wakimpongeza kwa ustadi wake katika suala la malezi na kama kawaida, kunao wengine waliokuwa na mambo mabaya ya kusema kuhusu picha ambayo alichapisha.

Shabiki mmoja alitilia shaka mapenzi yake kwa msichana huyo wa miezi mitatu kutokana na jinsi alivyomshikilia na hata kumtaka amfanyie vipimo vya DNA ili kuthibitisha kuwa ni binti yake halisi.

"Mtoto mweupe wewe na bibi weusi titititi! Mtoto alitoa Wapi weupe ??? DNA inahitajika haraka. Shida ya kupata mtoto uzeeni, huna hamu na mtoto. Jinsi unavyomshikilia mtoto, haujali. Sura yako na ya Huyo mtoto hazi ambatani . Maskio ya mtoto na yako haifanani, mapua na mdomo wa mtoto haikufanani.

Utatuaminishaje mtoto ni wako?? Sio mshangao kuona jinsi unavyomshika bila kujali. Acha kulea mtoto wa mwanaume mwingine. Ukweli unauma! Mkimaliza Matusi muende kazini. Wale wataleta hisia hapa wengi ni wanawake kwa sababu wanalazimisha wanaume kulea watoto sio wao ! Wale wanaume mtaleta feelings hapa mnalea watoto sio wenu ! DNA ni nafuu sasa nenda ukafanye vipimo," mtumizi wa FB alimwambia.

Nameless alicheka maoni hayo na kudokeza kuwa huenda mwanamitandao huyo anasumbuliwa na hali inayohitaji matibabu maalum.

"Hii lazima ni akaunti feki. Mwangalieni huyu sasa. Sasa unasemaje? Enda therapy wewe. Unahitaji tu upendo kidogo na mwelekeo na utakuwa sawa. Nigekusaidia lakini yako inahitaji usaidizi wa kitaalamu. Alafu onyesha daktari maoni haya yako atapatia dawa ya ugonjwa huu," alijibu.

Nameless na mkewe Wahu Kagwi wamekuwa wakipokea upendo na chuki nyingi tangu walipomkaribisha duniani mtoto wao wa tatu mwaka jana.