"Nimezama kwenye mahaba!" Ringtone Apoko afunguka kuhusu mahusiano mapya

Mwimbaji huyo alibainisha kuwa mapenzi yake mapya ni matamu sana.

Muhtasari

•Ringtone alitangaza habari hizo njema katika video aliyochapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumatatu.

•Alisema kuwa anafurahi sana kwa mahusiano yake mapya na kubainisha kuwa hakuwahi kufikiria kwamba atapata mapenzi.

Image: INSTAGRAM// RINGTONE APOKO

Mwimbaji maarufu wa nyimbo za injili Alex 'Ringtone' Apoko hatimaye amefanikiwa kupata kipenzi cha maisha yake.

Ringtone alitangaza habari hizo njema katika video aliyochapisha kwenye ukurasa wake wa Instagram siku ya Jumatatu.

Katika klipu hiyo fupi, mwanamuziki huyo aliyezingirwa na utata mwingi alidai kuwa amezama ndani kabisa kwenye mahaba.

"Nafurahi sana. Mazee nimezama kwenye mahaba. Nashukuru Mungu kwa kunisaidia kuzama kwenye mapenzi," alisema.

Mwenyekiti huyo wa kujitangaza wa Muungano wa Wasanii wa Injili wa Kenya alibainisha kuwa mapenzi yake mapya ni matamu sana.

Alisema kuwa anafurahi sana kwa mahusiano yake mapya na kubainisha kuwa hakuwahi kufikiria kwamba atapata mapenzi.

"Hivi karibuni nitawatambulisha kwa mpenzi wangu. Nimeanguka katika mapenzi mazee," alisema.

Aidha aliwashukuru mashabiki wake kwa kumuombea hadi akafanikiwa kupata mpenzi na kujikita katika mahusiano.

Haya yanajiri wiki chache tu baada ya mwimbaji mwenzake ambaye amekuwa akimmezea mate kwa muda mrefu, Justina Syokau kuweka wazi kwamba amekataa tamaa ya kuwa mke wake na hamtaki tena.

Mapema mwezi huu, mwanamuziki huyo mwenye mbwembwe nyingi alikanusha kuwa alikuwa anamtamani Ringtone.

 Kulingana naye, aliposema kuwa alikuwa anamtamani kimapenzi mwimbaji huyo mwenzake, hakuwa na maana kuwa alimtaka yeye bali alikuwa anataka maisha ya kifahari ya Runda na pesa za msanii huyo.

Justina alisema kuwa alimsikia Ringtone akisema ana upweke ndio maana akasema alikuwa anamtaka lakini uhalisia ni kwamba alikuwa anatamani kuishi Runda chini ya paa la Ringtone wala si mapenzi.

“Mwenyekiti wa Injili alisema ako upweke Runda, mimi nikasema sijafika Runda, mimi kusema kuwa nilikuwa namtamani kimapenzi Ringtone haikuwa na maana kuwa ni yeye, nilikuwa natamani Runda, na pesa. Si Ringtone kwa sababu mimi sina haja na yeye bali nilikuwa na haja na maisha ya Runda na pesa. Simhitaji Ringtone, sema tu nimechoka kulipa kodi ya kila mwezi kwa nyumba,”  alisema.

Mwaka wa 2019, Ringtone alizamia barabarani akiwa amebeba bango kubwa lenye maandishi ya sifa anazozingatia kwa mke.

Mwimbaji huyo aliweka wazi kuwa yuko tayari kutulia na alikuwa akitafuta mwanamke mzuri wa kutulia naye.