Diamond awasisimua wanafamilia baada ya kumtambulisha Zuchu kama mke wake

Diamond ni miongoni mwa wageni waliofika kwenye karamu ya Esma.

Muhtasari

•Diamond alimwalika mmoja wa wasanii wake, Zuhura Othman almaarufu Zuchu ambaye alitambulisha kama mwenzake.

•Kabla ya kuondoka jukwaani na kuchukua nafasi yake, mwimbaji huyo pia alimtaja Zuchu kama  wifi wa dada yake Esma.

ZUCHU NA DIAMOND PLATNUMZ
Image: WASAFI/INSTAGRAM

Dada mkubwa wa staa wa Bongo Diamond Platnumz, Esma Khan alisherehekea siku yake ya kuzaliwa Alhamisi, Februari 2.

Jioni hiyo, Esma ambaye alikuwa anatimiza miaka 37 aliandaa karamu ya kifahari ambayo ilihudhuriwa na wanafamilia, marafiki na watu wengine wa karibu. Diamond ni miongoni mwa wageni waliofika kwenye karamu ya Esma.

Baada ya kutoa hotuba yake  na kumwaga hisia zake kwa dadake kwenye karamu hiyo, bosi huyo wa WCB alimwalika mmoja wa wasanii wake, Zuhura Othman almaarufu Zuchu ambaye alitambulisha kama mwenzake.

"Sasa mwenzangu Zuhura akasema angependa sana tukuje pamoja. Sasa mimi ni shabiki wa maagizo naomba aje awasilishe," Diamond alisema huku chumba cha sherehe kikijawa na shangwe na nderemo.

Kabla ya kuondoka jukwaani na kuchukua nafasi yake, mwimbaji huyo pia alimtaja Zuchu kama  wifi wa dada yake Esma.

"Hapo ndipo tutajua kama ana mapenzi na wifi wake," alisema.

Wahudhuriaji wa karamu hiyo walionekana kufurahishwa sana na utambulisho wa Diamond kwa Zuchu, ishara ya wazi kuwa wengi wao wameidhinisha uhusiano kati ya wawili hao.

Esma hata hivyo alionekana kuwa na furaha zaidi wakati malkia huyo wa bongofleva, mzaliwa wa Zanzibar akienda jukwaani na kusimama kando yake.

"Tungepeenda kuskia upendo wako," mfawidhi wa karamu hiyo alimwambia Zuchu kupigwa na butwaa kutokana na upendo aliooneshwa.

Picha na video zingine za karamu hiyo zinamuonyesha binti huyo wa Khadija Kopa akijivinjari na kuburudika pamoja na Diamond, Esma na wengine ambao walikuwa wamehudhuria. Alionekana mwenye furaha kubwa sana kuwa pale.

Kwa muda mrefu wa zaidi ya mwaka mmoja, Zuchu amekuwa akidaiwa kutoka kimapenzi na  bosi wake Diamond Platnumz.

Wiki chache zilizopita hata hivyo, mamake Zuchu, Khadija Kopa alisisitiza kuwa bintiye yuko single kwani bado hajachumbiwa.

Kulingana na malkia huyo wa mipasho ya Taarab, bintiye hachumbiani na msanii Diamond kama ambavyo wengi wamekuwa wakiaminishwa kwa muda mrefu wa zaidi ya mwaka mmoja na miezi kadhaa sasa.

Kopa alisema kuwa kutokana na umaarufu wa Zuchu, siku akipata mchumba dunia nzima itajua na itakuwa ni habari ya mijini na vijijini, ila kwa sasa akawataka watu kuwa na subira na kutopotoshwa na kile ambacho wamekuwa wakikisikia mitandoani na kwenye mablogu ya udaku.

Zuchu bado yupo single, hana Mpenzi wala Mchumba na wala hajanitambulisha kwa Mwanaume yoyote kwamba Mama huyu ndiye Mwanaume wangu, Zuchu ni maarufu hata mimi Mama yake ni maarufu siku atakapopata Mchumba akanitambulisha matajua tu muwe na subira,”  alisema Khadija Kopa.

Mwaka jana, Zuchu na Diamond walidokeza kuwa kuna kitu kinachoendelea kati yao kutokana na matendo yao pamoja. Wawili hao walionekana wakijivinjari, kudensi pamoja, kuzawadiana na hata kubusus hadharani.