"Mtoto wangu" Mama Dangote ajivunia baada ya Diamond kumnunulia saa ya thamani

Saa hiyo yenye mapambo mengi inakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi nusu milioni za Kenya.

Muhtasari

•Siku ya Ijumaa, Mama Dangote alionyesha saa maridadi aina ya Hublot Geneve kwenye mkono wake na kufichua kuwa mwanawe alimnunulia.

•Mapema wiki hii, Diamond alionyesha mapenzi makubwa kwa msanii wake Zuchu kwa kumnunulia pambo la bei ghali.

Mama Dangote, Diamond Platnumz, Esma Platnumz
Image: INSTAGRAM// ESMA PLATNUMZ

Bi Sanura Kassim almaarufu Mama Dangote ni mwanamke mwenye raha baada ya mwanawe Diamond Platnumz kumzawadi saa ya thamani.

Siku ya Ijumaa, Mama Dangote alionyesha saa maridadi aina ya Hublot Geneve kwenye mkono wake na kufichua kuwa mwanawe alimnunulia.

"Mtoto wangu," aliandika chini ya video hiyo.

Saa hiyo yenye mapambo na madoido mengi inakadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi nusu milioni za Kenya.

Diamond anafahamika kuwa na uhusiano wa karibu mno na mzazi huyo wake na amemnunulia zawadi ghali mara nyingi.

Mapema wiki hii, bosi huyo wa WCB alionyesha mapenzi makubwa kwa msanii wake Zuchu kwa kumnunulia pambo la bei ghali.

Staa huyo wa Bongo ambaye kwa sasa yuko  Uingereza alionekana kwenye video akiwa ameshika cheni maridadi ya fedha yenye kichwa cha malkia ambayo alinunua katika duka moja la mapambo jijini humo.

Kulingana na taarifa kwenye ukurasa rasmi wa Wasafi, alinunua cheni hiyo inayomeremeta maalum kwa Zuchu.

"Simba amenunulia Zuchu pambo jipya kabisa jijini London," taarifa hiyo ilisoma.

Wimbo wao 'Mtasubiri' ambao unawasuta wanaochukia uhusiano wao uliambatanishwa na video hiyo.

Haya yalitokea siku chache tu baada ya bosi huyo wa WCB kuthibitisha kutengana na binti huyo wa Khadija Kopa.

Katika taarifa yake kwenye ukurasa wake wa Instagram, staa huyo wa Bongofleva aliweka wazi kwamba yeye na Zuchu sio wapenzi tena.

Diamond alibainisha kuwa yeye na malkia huyo wamebaki kuwa kaka na dada licha ya awali kuonyesha mahaba makubwa  kati yao.

"Kwa pamoja na Zuhura tunaomba tuwataarifu ya kwamba, kwa sasa sisi ni dada na kaka na si wapenzi kama ilivyokuwa ikidhaniwa ama wengine kujua.. Mnaruhusiwa wachumba na wake ama waume kama tutawaridhia," alisema.

Diamond aliongeza, "Lakini muwe na vibarua vinavyoeleweka  sio mje kutuchuna, maana atuhongi hovyo."

Hapo awali, Zuchu aliibua wasiwasi juu ya hali ya mahusiano yao kufuatia chapisho lake kwenye mtandao wa Snapchat.

Mwimbaji huyo wa kibao 'sukari' alidokeza kwamba amevunjwa moyo na mpenzi wake na kutangaza kuwa yuko single.

"Single.." aliandika na kuambatanisha na emoji ya moyo uliovunjika '💔'

Binti huyo wa Khadija Kopa pia alichukua hatua ya kufuta picha zote za bosi wake Diamond kwenye mtandao wa Instagram.