Karen Nyamu ajibu kuhusu kummezea mate gavana Sakaja

"Wa Wairimu wewe unataka kuchukua Sakaja pia," Nyamu aliulizwa.

Muhtasari

•Nyamu aliungana na gavana wa Nairobi, Johnson Sakaja wakati wa uzinduzi wa chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Mama Lucy siku ya Jumatano.

•Shabiki mmoja alibaini jinsi Nyamu alivyomimina sifa tele kwa gavana huyo na akamuuliza ikiwa anavutiwa naye.

Seneta Karen Nyamu akimkumbatia gavana wa Nairobi Johnson Sakaja
Image: HISANI

Seneta wa kuteuliwa Karen Njeri Nyamu aliungana na gavana wa kaunti ya Nairobi, Johnson Sakaja wakati wa uzinduzi wa chumba cha wagonjwa mahututi katika hospitali ya Mama Lucy siku ya Jumatano.

Katika taarifa yake baada ya uzinduzi, wakili huyo alimpongeza Sakaja kwa kupatia kipaumbele huduma za afya katika Kaunti ya Nairobi.

"Asante gavana Sakaja Johnson kwa kutanguliza huduma za afya jijini Nairobi. Kadri idadi ya wagonjwa katika hospitali za umma inavyoongezeka kutokana na kuboreshwa kwa sekta ya afya ya umma, tafadhali tupe wauguzi zaidi, madaktari, teknolojia ya Maabara, Maafisa wa Afya ya Umma na wataalamu wa lishe ili kuhakikisha huduma kwa wakati," aliandika kwenye ukurasa wake wa Facebook Jumatano.

Aliambatanisha taarifa hiyo na video yake pamoja na Sakaja na viongozi wengine akitoa hotuba wakati wa hafla hiyo.

Shabiki mmoja alibaini jinsi Nyamu alivyomimina sifa tele kwa gavana huyo na akamuuliza ikiwa anavutiwa naye.

"Wa Wairimu wewe unataka kuchukua Sakaja pia," Njiema Mwenda alimuuliza seneta huyo wa chama cha UDA.

Nyamu bila kusita alijibu, "Hapana!"

Hivi majuzi, mwanasiasa huyo aliandamana na mzazi mwenzake Samuel Muchoki almaarufu Samidoh kuhudhuria mazishi ya mpwa wake, Geoffrey Mwathi Ngugi, ambapo mwimbaji huyo alimtambulisha mbele ya familia.

Samidoh alijitambulisha kama mjomba wa marehemu kabla ya kumualika Nyamu kuwasalimia waombolezaji na kuwafariji.

"Kuja Mama Wairimu usalimie watu. Kuja usalimie watu kisha turejeshe kipaza sauti kwa MC,"  alisema mwimbaji huyo.

Nyamu alitumia fursa hiyo kuwafariki waombolezaji na kuwatia nguvu waweze kukabiliana na majonzi ya kumpoteza mpendwa wao.

"Mimi naitwa Karen Njeri.Kama mlivyosikia, mimi ni seneta. Leo nashirikiana na nyinyi katika siku hii ya huzuni. Hatutamlalamikia Mungu. Hivyo ndivyo Mungu alikuwa amepanga. Tukienda juu tutakutana naye," alisema.

Wawili hao wamekuwa kwenye mahusiano tatanishi kwa muda mrefu na tayari wamebarikiwa na watoto wawili pamoja.