Esther Musila alalamika kutongozwa na wanaume wengi mitandaoni licha ya kuwa ameolewa

Musila alisema kuna wanaume wengi ambao wako tayari kuangusha ndoa yake na Guardian Angel.

Muhtasari

•Esther Musila amefichua kwamba kuna wanaume wengi ambao wamekuwa wakijaribu kumtongoza kwa jumbe tamu za mapenzi licha ya yeye kuwa kwenye ndoa tayari.

•Guardian Angel pia alifichua kwamba kuna wanadada wengi wanaojaribu kumtongoza kupitia kwenye mitandao ya kijamii.

Esther Musila na mume wake Guardian Angel
Image: INSTAGRAM// ESTHER MUSILA

Mke wa mwimbaji wa nyimbo za injili Guardian Angel, Esther Musila amefichua kwamba kuna wanaume wengi ambao wamekuwa wakijaribu kumtongoza kwa jumbe tamu za mapenzi licha ya yeye kuwa kwenye ndoa tayari.

Akizungumza na waandishi wa habari, mama huyo wa watoto watatu wakubwa alieleza kuwa kurasa zake za mitandao ya kijamii zimejaa jumbe tamu za mahaba kutoka kwa wanaume ambao wamekuwa wakimmezea mate.

Musila hata hivyo aliweka wazi kwamba huwa anapuuza jumbe hizo na hata kufuta baadhi yake ambazo zimepita mipaka.

"Huwa zinakuja (Jumbe) lakini huwa nazipuuza tu. Zile ambazo zimekithiri huwa nafuta na kublock," alisema.

Alisema kuna wanaume wengi ambao wako tayari sana kuangusha ndoa yake ya zaidi ya mwaka mmoja na Guardian Angel.

"Ni wengi sana. Lakini hakuna nafasi ya kuwatumbuiza," alisema.

Guardian Angel pia alifichua kwamba kuna wanadada wengi wanaojaribu kumtongoza kupitia kwenye mitandao ya kijamii.

Hata hivyo, alisema kwa kawaida huwapuuza au hata kuwablock watumaji kwani yuko kwenye ndoa yenye furaha na Musila.

"Mimi nawaruhusu kunipenda. Lakini ikifika kwa upendo wa kindoa, tayari nina pete. Si kwa sababu ya pete tu, niko na mtu ninayependa  kindoa. Ile upendo ingine ya kawaida naruhusu kabisa, lakini ya kindoa, niko hapa nafurahi," alisema.

Mwimbaji huyo mahiri alifutilia mbali uwezekano wa yeye kuoa mke wa pili huku akiweka wazi kuwa ameridhika sana na mkewe Esther Musila.

Guardian Angel alikiri kwamba inaweza kuwa vigumu kwake kuwezana na wanawake wawili kwani Bi Musila pekee yake humchokesha wakati mwingine.

"Neema yangu hainiruhusu, sina huo uwezo. Hata huyu mmoja saa zingine ni mzigo kidogo. Mwanamke mmoja tu pia sio mchezo. Majukumu ya huyu mmoja sio mchezo," alisema.

Aidha, alibainisha kuwa baadhi ya watangulizi wake katika familia yao walikuwa na wake zaidi ya mmoja lakini haikuishia vyema kwao.

Wanandoa hao wamekuwa pamoja kwa takriban miaka minne na walifunga pingu za maisha mapema mwaka jana. Ndoa yao hata hivyo imekuwa ikikosolewa sana haswa kutokana na pengo kubwa kati ya umri wao.

Bi Musila ana umri wa miaka 53 na ana watoto watatu wakubwa kutoka kwa ndoa yake ya awali huku Guardian Angel akiwa na miaka 33. Hakuna habari zozote zilizo wazi kuhusu familia nyingine ya msanii huyo ikiwa ipo.