"Huwezi zaa nami ukatia huruma" Harmonize amuahidi mzazi mwenzake nyumba, gari na biashara

Konde Boy aliweka wazi huwa hachukulii upendo wa Shanteel kuwa za kawaida tu.

Muhtasari

•Siku ya Jumatano, Shanteel aliandika ujumbe mzuri wa siku ya kuzaliwa kwa mwimbaji huyo kwa niaba ya binti yake.

•Bosi huyo wa Kondegang alidokeza kuwa mzazi huyo mwenzake amekuwa akitamani wawe pamoja.

Official Shanteel na Harmonize
Image: INSTAGRAM

Staa wa Bongo Rajab Abdul Kahali almaarufu Harmonize amemlimbikizia sifa kemkem mzazi mwenzake, Official Shanteel baada ya kutumia ukurasa wa binti yao Zuuh Konde kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa.

Siku ya Jumatano, Shanteel aliandika ujumbe mzuri wa siku ya kuzaliwa kwa mwimbaji huyo kwa niaba ya binti yake. Katika ujumbe huo, Zuuh alitambua uwepo wa babake katika maisha yake na muungano wao mzuri.

"Kheri ya Siku ya Kuzaliwa Baba! Shukran kwa kila kitu ulichonipa. Kila siku uko kwa ajili yangu baba na rafiki bora pia. Hakuna muungano mwingine kama wetu. Nakupenda baba @harmonize_tz," ujumbe ulisomeka. 

Konde Boy alibainisha kuwa mzazi mwenzake ndiye aliyemwandikia binti yao ujumbe huo na hivyo kutoa shukrani kwake.

"Mama Zurekha asante kwa kugusa maisha yangu. Najua Zuu hawezi kuandika haya yote ila  hii ina maana kubwa sana kwangu." alisema.

Wakati huohuo, bosi huyo wa Kondegang alidokeza kuwa mzazi huyo mwenzake amekuwa akitamani wawe pamoja. Pia aliweka wazi kuwa kamwe huwa hachukulii upendo wa Shanteel kuwa za kawaida tu.

 "Zuuh akishakuwa mkubwa ataona na kujua kwa kiasi  gani ulitamani wazazi wake tuwe pamoja!!!  Ingawa ukipanga na Mungu Mtukufu anapanga. Kama ilivyo wazi, hatujawahi kwa wapenzi kiivyo lakini nakuahidi maisha yamenifundisha kukuona wa thamani na nastahili kubadilisha maisha yako kama ulivyofanya niitwe baba,"

Kufuatia hayo, Kondeboy  aliahidi kumtuza mzazi huyo mwenzake kwa gari, nyumba na biashara katika kipindi cha miezi miwili ijayo.

"Huwezi zaa na Konde ukawa unatia huruma. Hata nisipokuwa na Hela watu wananipenda saana siwezi shindwa vitu vidogo," alisema.

Staa huyo wa Bongo alisherehekea kutimiza miaka 29 mnamo Jumatano, Machi 15.

Ingawa haijulikani kabisa kama waliwahi kuchumbiana rasmi, Harmonize na Official Shanteel walishiriki kitu pamoja ambacho kilipelekea kuzaliwa kwa binti yao mrembo,  Zuuh Konde mwaka wa  2019. Zuuh ni mtoto wa pekee wa mwanamuziki huyo wa Bongo ambaye anajulikana.