Mwanamume atunukiwa 100K kwa kuibuka mshinda katika shindano la kula

Mwanamume huyo alitumia dakika 8 na sekunde 6 kumaliza kula wali na nyama kilo mbili pamoja na maji lita moja.

Muhtasari

• Baada ya kumaliza kula, mwanamume huyo alitunukiwa laki moja na yoghurt mbili.

• Shindano la Tonge Nyama lilikuwa linafanyika kwa awamu ya 9, na lengo lake ni kuhimiza uzalendo.

David Shaoti, mshindi wa shindano la kula.
David Shaoti, mshindi wa shindano la kula.
Image: Ayo Tv

Kijana mmoja wa kiume aliyetumia dakika 8 tu kula wali kilo mbili hadi kuumaliza kavu atunukiwa shilingi laki moja pesa za        Tanzania, sawa na shilingi 5500 pesa za Kenya.

Mchezo huo wa mashindano ya kula ambao ni pendwa kwa wakaazi wa Morogoro nchini humo ulifanyika wikendi iliyopita na mamia ya wakaazi wa mji huo walijitokeza kushuhudia namna wapambanaji wa kula walishiriki mchezo huo.

Shindano hilo maarufu kwa jina la Tonge Nyama liliwavutia washiriki watano walitinga ulingoni kupambana katika ulaji wa wali na nyama kilo mbili na maji lita moja.

Mshindi huyo aliyetambuliwa kwa jina David Shaoti aliibuka mshindi baada ya kutumia dakika nane na sekunde sita kumaliza chakula hicho.

Katika kinyang’anyiro hicho, mamia walikuwa wakiwasherehekea wapambanaji wao kama utimu vile huu shughuli hiyo ikipambwa na mshereheshaji ambaye alikuwa akiwapa motisha washidnani kwa kuradidi maneno ‘usiache kula’

Kando na mshereheshaji, pia kulikuwa na muziki ambao ulikuwa unawapa motisha na walionekana wakimenyana kwa kubugia wali mdomoni huku wakitikiza vichwa kwa midundo ya muziki huo.

Mshindi huyo baada ya kufagia sinia lake, alinyoosha mkono pia na kuanza kumsaidia mwenzake kula wali ule.

Katika kuzungumza na wanahabari baada ya kutunukiwa ushindi, Shaoti aliwahimiza vijana wengine kujitokeza kwa wingi na kushiriki mchezo huo kwani ni kama mchezo mwingine ila akatoa tahadhari moja – kufanya mazoezi kwa wingi.

“Baada ya kushinda mchezo huu nimetunukiwa shilingi laki moja na yoghut mbili. Mazoezi ambayo mtu anaweza kufanya ni kukimbia na pia kushiriki gym ili kumweka mtu vizuri katika kushiriki mchezo huu katika kupata hamu ya kula,” alisema.

Lengo la shindano hilo ni kuwafikia vijana wa mitaani ili kuhamasisha uzalendo na kupiga vita unyanyasaji wa kijinsia.