Eric Omondi akamatwa tena akiandamana na kutishia kujinyonga jijini Nairobi (+video)

"Mimi nitajiua hapa. Mimi leo nitaruka hapa na hii kamba ininyonge na nizikwe," alisema.

Muhtasari

•Eric anaendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Central baada ya kukamatwa na maafisa siku ya Jumatatu asubuhi.

•Eric alitishia kujitia kitanzi kama njia ya kuishinikiza serikali ya Kenya kupunguza gharama ya maisha.

amekamatwa akiandamana jijini Nairobi
Eric Omondi amekamatwa akiandamana jijini Nairobi
Image: HISANI

Mchekeshaji aliyegeuka kuwa mwanaharakati, Eric Omondi , ametiwa mbaroni kwa mara nyingine baada ya kuandamana jijini Nairobi.

Eric anaendelea kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Central baada ya kukamatwa na maafisa siku ya Jumatatu asubuhi. Alikuwa akiandamana dhidi ya gharama ya juu ya maisha wakati ambapo alikamatwa.

Huku akiwa amejihami na kipaza sauti mkononi na kamba shingoni, Eric alisimama kwenye jukwaa ambalo alisimamisha katikati mwa jiji.

"Natoka hapa nikiwa nimekufa leo ndio sauti ya Mkenya mnyonge isikike. Mimi nitajinyonga ndio mnyonge asikike," alisikika akisema.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 41 alisikika akiimba wimbo wa Juliani, 'Utawala' ambao unahusu kukosoa utawala mbovu.

"Niko njaa hata siezi karanga

Hoehae shaghala bhaghala

Niko tayari kulipa gharama

Sitasimama maovu yakitawala

Sitasimama maovu yakitawala," aliimba huku kundi ndogo la watu wakiwa wamesimama huku wakimtazama.

Eric alitishia kujirusha kutoka kwenye jukwaa alilokuwa amesimama juu yake na kujitoa uhai kutumia kamba iliyokuwa shingoni kama njia ya kuishinikiza serikali ya Kenya kupunguza gharama ya maisha.

"Sauti ya Mkenya lazima itasikika, sauti ya mwananchi itasikika. Mimi nitajiua hapa leo. Mimi leo nitaruka hapa na hii kamba ininyonge na nizikwe. Lakini bei ya unga itaenda chini," Eric alisikika akisema.

Kabla ya kutiwa mbaroni, mchekeshaji huyo mahiri alisikika akimweleza afisa wa polisi sababu yake ya kuandamana.

Kizaazaa kikubwa kilizuka huku maafisa hao wakijaribu kumshawishi mchekeshaji huyo ashuke kabla ya kumchukua . Milio ya bunduki ya kutupa vitoa machozi ilisikika huku umati uliokuwa umekusanyika pale ukitawanywa.

Hii ni mara ya nne ya mchekeshaji huyo mkongwe kukamatwa katika kipindi cha miezi miwili iliyopita. Hapo awali alikamatwa mara tatu kuhusiana na maandamano dhidi ya gharama ya juu ya maisha.

Jumanne wiki iliyopita, alikamatwa kwa mara ya tatu akielekea Ikulu.

Eric alikuwa akivuta mkokoteni wa mbao aliodai kuwa umebeba maelfu ya CV za vijana wanaotafuta kazi. Nia yake kuu ilikuwa ni kuziwasilisha Ikulu.

Wakati akivuta mkokoteni wake, mchekeshaji huyo pia alikosoa serikali kwa kutobuni nafasi za kazi kwa mamilioni ya Wakenya.

Omondi alitaka kumpa Rais William Ruto CV hizo ili kumuonyesha jinsi ukosefu wa kazi ulivyokuwa tatizo nchini.

"Mimi staki kuweka maisha ya watu hatarini. Mimi nilienda nicacollect CVs, ziko hapa 3 million napelekea mheshimiwa William Samoei Ruto aone watu wake wenye wameenda university na hawana kazi," alisema.

Hata hivyo, alikamatwa katika Barabara Kuu ya Uhuru na kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi.