Fahamu jinsi Akothee alivyokutana na mume wake Denis Schweizer

Wawili hao walikutana Julai 16 katika kikao cha biashara kilichoandaliwa na rafiki yao.

Muhtasari

•Akothee na Schweizer walifunga pingu za maisha katika harusi ya kifahari iliyofanyika Windsor Golf Hotel & Country Club, Nairobi siku ya Jumatatu.

•"Tulienda kupimwa UKIMWI kabla ya chochote. Baada ya wiki tatu, alinitambulisha kwa familia na marafiki zake, Omosh ana familia nzuri, nilikwama hapo" Akothee alisimulia.

Akothee na mume wake Denis Shweizer
Image: INSTAGRAM// AKOTHEE

Mwimbaji Esther Akoth almaarufu Akothee na mchumba wake Dennis Shweizer almaarufu Mister Omosh walifunga pingu za maisha katika harusi ya kifahari iliyofanyika Windsor Golf Hotel & Country Club, Nairobi siku ya Jumatatu.

Harusi ya pili ya mama huyo wa watoto watano ilipambwa na wanafamilia, marafiki wa karibu, wasanii maarufu na wanasiasa mashuhuri nchini. Jumla ya watu wasiopungua 300 walikuwa wamealikwa kwenye hafla hiyo ya kufana.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 amekuwa gumzo kuu kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii tangu harusi hiyo kufanyika mnamo Aprili 10 huku wengi wakionekana kumuangazia zaidi mume wake Denis Shweizer. Wakenya wengi wamekuwa na shauku kubwa ya kutaka kujua mzungu huyu asiyeeleweka ni nani, anafanya kazi gani na jinsi alivyokuja kukutana na mama huyo wa watoto watano.

Hakuna maelezo zaidi kuhusu kazi ya Bw Shweizer lakini wakati walipoanza kuchumbiana mwaka jana, Akothee alimtambulisha mzungu huyo kama mwenyekiti mpya wa wakfu wake, The Akothee Foundation.

Takriban miezi mitano iliyopita, mwanamuziki huyo alisimulia hadithi ya jinsi alivyokutana na raia huyo wa Uswizi.  Akothee alifichua kuwa alikutana na mzungu huyo katika Ziwa Zug, nchini Uswizi mnamo Julai 16, 2022.

Alifichua kuwa walijipata na mume huyo wake katika na  kikao cha kibiashara ambacho kilikuwa kimeandaliwa na rafiki yao mmoja na baadaye Omosh akachukua simu yake na kusave namba yake kama 'Mume Wangu'

"Tulienda kuogelea kwenye ziwa Zug na baadaye tukarudi nyumbani. Kitu cha kuchekesha kilitokea, sisi sote tulikuwa tumevutiana sana, sikuwa na namba yake lakini alikuwa na yangu, kwani alisave yake kwenye simu yangu na akapiga simu yake."

Kisha baadae akampigia simu rafiki yake na kusema anataka kuongea na mimi kwenye video call, tukazungumza, kisha akaniuliza,  nimpigie na simu yangu, na nikamwambia kuwa sina namba yake," alisimulia.

Akothee alisema alishtuka sana baada ya kugundua kuwa mzungu huyo alijisave kama 'Mume wangu' kwenye simu yake.

Alisema baada ya wao kufahamiana ,Omosh alianza kumwonyesha mahaba mazito na kumdekeza kama msichana mdogo, jambo ambalo hakuwahi kushuhudia na mwanamume yeyote aliyewahi kuchumbiana naye hapo awali.

"Tulienda kupimwa UKIMWI kabla ya chochote. Na baada ya wiki tatu, alinitambulisha kwa familia na marafiki zake, Omosh ana familia nzuri, nilikwama hapo"

Mwimbaji huyo alisema siku ambayo mpenzi wake alimchumbia na kumvisha pete ya uchumba hakuamini na alifikiri alikuwa akiota .

Alisema mwanzoni hakupanga kuweka mahusiano yao hadharani lakini aligundua hangeweza kuficha kwa muda mrefu kwa  kuwa yeye ni mtu maarufu  na hakutaka watu wachanganye mpenziwe na watu wengine.