Andrew Kibe alalamika kwa uchungu kwa kutoalikwa kwenye harusi ya Kamene Goro

"Naweza anza kutoa machozi hapa. Mbona hukunitumia mwaliko wa harusi," alilalamika.

Muhtasari

• Kibe alilalamika kuwa mtangazaji mwenzake huyo wa zamani hakumwalika kwenye hafla hiyo  licha ya kufanya naye kazi hapo awali.

•"Mtu tulifanya kazi na yeye bro. Mtu nilienda nikamtetea mshahara nikasema tafadhali mpatie nyongeza," Kibe alilalamika.

Kamene Goro, Andrew Kibe na, DJ Bonez
Image: HISANI

Muundaji maudhui Andrew Kibe ameibua malalamishi dhidi ya mwenzake wa zamani Kamene Goro kwa kutomwalika kwenye harusi yake.

Kamene Goro alifunga pingu za maisha na mpenzi wake David Pyper almaarufu Deejay Bonez siku ya Alhamisi katika harusi ya faragha iliyohudhuriwa na wanafamilia kadhaa na marafiki wachache wa karibu.

Akizungumza wakati wa kipindi cha moja kwa moja siku ya Alhamisi jioni, Kibe alilalamika kuwa mtangazaji mwenzake huyo wa zamani hakumwalika kwenye hafla hiyo  licha ya kufanya naye kazi hapo awali.

"Mtu tulifanya kazi na yeye bro. Mtu nilienda nikamtetea mshahara nikasema tafadhali mpatie nyongeza," Kibe alisema.

Mtumbuizaji huyo ambaye kwa sasa anaishi Marekani aliweka wazi kwamba kutoalikwa kwenye harusi hiyo kulimvunja moyo.

"Naweza anza kutoa machozi hapa. Mbona hukunitumia mwaliko wa harusi," alilalamika.

Kibe pia alishangaa kwa nini kipusa huyo mwenye umri wa miaka 30 alimchagua mcheza santuri kuwa mwenzi wa maisha.

Kamene Goro na mpenzi wake wa muda mrefu DJ Bonez waliripotiwa kuvishana pete za ndoa Alhamisi katika hafla ya faragha.

Mbunge wa eneo la Lang’ata, ambaye ni rafiki wa karibu sana na mtangazaji mwenza wa zamani wa Kamene Goro alishiriki picha na video za tukio zima kwenye ukurasa wake wa Instagram na kuwapongeza wawili hao.

"Mapenzi ni kitu kizuri! Hongera sana dada yangu @kamenegoro na @deejaybonez254 kwenye siku ya harusi yenu! Nawapenda wadau," alisema.

Mwaka jana, Kamene ilibidi ajitokeze na kutupilia mbali madai kwamba alikuwa amefunga ndoa  na mpenzi wake kwa siri baada ya tetesi kuibuka.

Wakati huo, mtangazaji huyo wa zamani wa redio alifafanua kwamba alikuwa mfawidhi kwenye harusi ya rafiki yake.

"Ni habari njema, habari nzuri lakini nataka kuweka rekodi sawa kwamba bado sijaolewa, labda nitakuwa mwaka ujao," alisema.

Kamene aliendelea kufichua kuwa alikuwa amechumbiwa rasmi.

"Hakukuwa na harusi ya siri, ilikuwa ni harusi ya rafiki yangu ambaye naenda kuwa MC. Hata hivyo, habari njema ni kwamba nilichumbiwa na ni muhimu kuweza kushiriki mambo makubwa yanazotokea katika maisha yetu," alieleza.

Taarifa za harusi hiyo zilichochewa na mfululizo wa machapisho aliyoweka akiwa na mpenzi wake DJ Bonez.