Zari afunguka kuhusu Shakib kuwa mlinzi wa zamani wa aliyekuwa mumewe, Ivan Ssemwanga

Alibainisha kuwa picha za Shakib na Ivan ambazo zimekuwa zikisambazwa zilipigwa wakati wakibarizi pamoja.

Muhtasari

•Katika siku za nyuma, picha za Shakib akiwa pamoja na Ivan  zilisambaa mitandaoni huku uvumi ukienezwa kuwa  aliwahi kufanya kazi ya kulinda lango kwenye makazi ya Ssemwanga nchini Afrika Kusini.

•"Kila mtu yuko huru kusema anachotaka. Huwezi kuwazuia. Mimi najua ukweli. Yeye (Zari) pia anajua ukweli," Shakib alisema.

amezungumzia madai ya mumewe, Shakib Cham Lutaaya, kuwa mlinzi wa zamani wa marehemu Ivan Ssemwanga
Zari Hassan amezungumzia madai ya mumewe, Shakib Cham Lutaaya, kuwa mlinzi wa zamani wa marehemu Ivan Ssemwanga
Image: HISANI

Mwanasosholaiti wa Uganda Zari Hassan hatimaye amejibu tetesi ambazo zimekuwepo nchini humo kwa muda mrefu kuwa mume wake Shakib Cham Lutaaya aliwahi kuwa mfanyikazi wa aliyekuwa mumewe, Ivan Ssemwanga.

Katika siku za nyuma, picha za Shakib akiwa pamoja na mzazi mwenza huyo wa Zari  zilisambaa mitandaoni huku uvumi ukienezwa kuwa  aliwahi kufanya kazi ya kulinda lango kwenye makazi ya Ssemwanga nchini Afrika Kusini.

Wakati akizungumza na waandashi wa habari siku ya Alhamisi, mama huyo wa watoto watano hata hivyo alizika tetesi hizo na kubainisha kuwa mume huyo wake mwenye umri wa miaka 31 hakuwahi kuajiriwa na marehemu Ivan.

"Tunahitaji kuzungumzia hili. Nimeona watu wakisema kwamba Shakib alikuwa mlinzi wetu, eti aliwahi kufanya kazi kwa Ivan. Ili kuweka mambo wazi, Shakib hajawahi kufanya kazi kwa Ivan," Zari Hassan alisema.

Alibainisha kuwa picha za Shakib na Ivan ambazo zimekuwa zikisambazwa zilipigwa wakati wakibarizi pamoja.

Mwanasosholaiti huyo mwenye umri wa miaka 42 aliamua kumwaga mtama baada ya mumewe kukwepa kuzungumzia madai hayo.

"Kila mtu yuko huru kusema anachotaka. Huwezi kuwazuia. Mimi najua ukweli. Yeye (Zari) pia anajua ukweli," Shakib alisema wakati alipoombwa kuzungumza kuhusu picha hizo na madai kuwa alikuwa mlinzi wa Ivan.

Mapema mwaka huu, Zari na Shakib walitembelea kaburi la marehemu Ivan Ssemwanga katika kijiji cha Nakaliro, katika Mji wa Kayunga, nchini Uganda. Wawili hao waliandamana na wengine kadhaa katika ziara hiyo.

Zari alirekodi video fupi ikimuonyesha akiwa amekaa kwenye kaburi hilo la baba ya watoto wake watatu wa kwanza huku watu wengine ambao walikuwa wameandamana naye wakipumzika kuzunguka eneo hilo.

Bw Ssemwanga, ambaye alikuwa mfanyibiashara tajika nchini Afrika Kusini alifariki katika hospitali ya Steve Biko Academic, jijini Pretoria, Afrika Kusini ambako alikuwa amekimbizwa akiwa katika hali mbaya.

Baadaye alizikwa kijijini kwao Nakaliro katika hafla ghali iliyohudhuriwa na watu maarufu na matajiri nchini Uganda na kwingineko ikiwa ni pamoja na wanamuziki Jose Chameleone, Bobi Wine, SK Mbuga na Weasel.

Ssemwanga ambaye alitambulika kama kiongozi wa Rich Gang nchini Uganda alifariki akiwa na umri wa miaka 39 na aliacha nyuma watoto watatu wa kiume ambao alikuwa amepata na mwanasoshalaiti Zari Hassan.

Wawili hao walikuwa kwenye ndoa kwa zaidi ya mwongo mmoja na kujaliwa watoto watatu pamoja kabla ya kutengana. Baadae Zari alijitosa kwenye mahusiano na Diamond na kupata watoto wengine wawili naye.