Kijana ashinda bet ya 10M kwa kutumia Ksh 130, babake amtaka kurudisha hela hizo

Kijana huyo alilalamika kwamba babake anapinga vikali kitu chochote kinachohusiana na kamari na hivyo aliweka wazi hawezi kuruhusu pesa za kamari katika boma lake.

Muhtasari

• Kijana huyo mwenye mawazo mtanange alishangaa cha kufanya kwani babake alikataa kuidhinisha pesa hizo kwenye boma lake licha ya kuoneshwa 'slip' ya kucheza.

Baba akataa kupokea kijanake nyumbani baada ya kushinda kamari, amtaka kurudisha hela hizo kwa kampuni ya ubashiri.
Baba akataa kupokea kijanake nyumbani baada ya kushinda kamari, amtaka kurudisha hela hizo kwa kampuni ya ubashiri.
Image: Maktaba

Kijana mmoja mwenye umri wa miaka 19 amebaki kwenye njia panda baada ya kushinda hela ndefu kutoka kwa mchezo wa Kamari lakini babake akazikataa hela hizo kwenye boma lake.

Kulingana na taarifa kutoka majarida ya Nigeria ambayo yalipata kisa hicho baada ya ndugu ya kijana huyo kuulizia msaada wa kimawazo mitandaoni, kijana huyo alikuwa amewekeza ‘mkeka’ kwenye Kamari ya mitandaoni akitumia Naira 450 ambacho ni sawa na shilingi 134 za Kenya.

Kwa bahati nzuri, kijana huyo wa miaka 19 alijishindia kima cha Naira milioni 38 ambacho ni kiasi sawa na shilingi milioni 11 pesa za Kenya.

Kwa furaha alikimbia nyumbani na kuwataarifu wazazi wake kuonekaniwa na nyota ya jaha, lakini baba mtu alikataa kumsikiliza akisema kuwa hawezi kuidhinisha pesa hizo katika boma lake, licha ya kuoneshwa dau lililoshinda kima hicho.

Kakake mshindi aliyebahatika kushiriki hadithi hiyo kwenye jukwaa la ujumbe la NGL, alifichua kuwa nduguye alishinda hela, lakini baba yao anasisitiza airudishe kwa kampuni ya kamari.

Kulingana naye, mwanamume huyo anapinga vikali chochote kinachohusiana na kamari, ndiyo maana anakataa kumruhusu mwanawe kushika pesa hizo kwa vile anajua ni kutokana na kamari za michezo.

“Kakangu wa miaka 19 alishinda N38M kwa kutumia naira 450 na baba yangu anasisitiza arudishe pesa kwenye michezo kwa sababu haungi mkono kucheza kamari licha ya kuelezea na kumwonyesha slip, bado anasisitiza. Kodi yetu inapaswa kulipwa baada ya miezi miwili, sasa imesababisha shida kati yake na mama. Naombeni ushauri mzuri,”

Hili linazua matatizo katika nyumba yao kwani mkewe amekasirishwa na uamuzi wake wa kutupilia mbali baraka haswa kwani kodi ya nyumba yao inadaiwa baada ya miezi michache.