Usiwe na haraka kuhama nyumbani kwa wazazi, maisha huku nje ni katili - DJ ashauri

Hata hivyo, yeye alisema kuwa japo anatoa ushauri huo, mwenyewe alitoka kwa wazazi wake mapema lakini akajitetea kwamba ni kutokana na hali ya kazi yake.

Muhtasari

• “Kwa nini una haraka sana kuondoka nyumbani kwa wazazi wako ikiwa una umri wa miaka 17 au 18?” VJ Adams aliulizwa.

DJ ashauri vijana kutokuwa na haraka kuhama nyumbani kwa wazazi
DJ ashauri vijana kutokuwa na haraka kuhama nyumbani kwa wazazi
Image: Instagram

Vijana wanashauriwa na mwanahabari maarufu kutoka nchini Ghana, VJ Adams wasiharakishe kuondoka nyumbani kwa wazazi wao.

 

Adams ambaye ana ufuasi na ushawishi mkubwa mitandaoni kando na kuwa mwanahabari pia ni DJ na Anaamini kuwa sio busara kwa vijana kuharakisha kujitenga kutoka nyumba za wazazi wao na kuanza maisha yao mbali na wazazi.

VJ Adams alisisitiza hitaji la vijana kuzingatia kwa umakini kukaa na wazazi wao hadi katikati mwa miaka ya 20 hadi mwishoni mwa miaka ya 20 ikiwa wana bahati ya kuishi katika vitongoji vya kifahari.

Alidai kuwa kwa kufanya hivyo, wataweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya ununuzi wa nyumba ya baadaye au kukodisha nyumba.

“Kwa nini una haraka sana kuondoka nyumbani kwa wazazi wako ikiwa una umri wa miaka 17 au 18?” VJ Adams aliulizwa.

“Fikiria jambo hilo. Katika miaka kumi ijayo, ukiwa na umri wa miaka 27, ukiweka akiba kiasi kila mwaka kana kwamba unalipa kodi ya nyumba, hiyo ingeongeza na hatimaye ujikimu. Kufikia wakati uko tayari kuhama, unaweza kununua nyumba au hata kukodisha ambayo unaweza kuandaa kwa kupenda kwako.” Aliongeza.

VJ Adams pia alishiriki kwamba yeye binafsi alihama kutoka kwa nyumba ya wazazi wake katika umri mdogo kwa sababu ya asili ya kazi yake.

Kauli hii yake ilizua maoni kinzani mtandaoni, baadhi wakisema alikuwa na wazo la busara na wengine wakimsuta kwa kile walisema anawashauri vibaya vijana ambao wanafaa kuanza kujitegemea mapema ili kuondoa mzigo kwa nyumba za wazazi pindi wanapo jitambua na kuzidi miaka 18.

Je, wewe maoni yako ni yepi kuhusu umri sahihi wa mtoto kuondoka katika nyumba ya mzazi?