"Siendi gym bure!" Akothee alitetea vikali vazi alilovaa wakati akitumbuiza nchini Uswidi

Akothee alibainisha kuwa anajivunia sana mwili wake ambao ameuweka sawa kwa kufanya mazoezi kwenye gym.

Muhtasari

•Akothee ametetea vazi lake la kutatanisha alilovaa jukwaani alipokuwa akitumbuiza jijini Stockholm, Uswidi wikendi iliyopita.

•Akothee ameeleza kwamba ili utumbuizaji wa muziki kwenye jukwaa uwe mzuri, ni lazima msanii avutie masikio na macho ya mashabiki.

Akothee akitumbuiza nchini Sweden wikendi.
Image: FACEBOOK// AKOTHEE

Mwimbaji Esther Akoth almaarufu Akothee ametetea vazi lake la kutatanisha alilovaa jukwaani alipokuwa akitumbuiza jijini Stockholm, Uswidi wikendi iliyopita.

Baada ya kuzichapisha kwa mara ya kwanza picha zake zilizopigwa wakati wa tamasha hilo kwenye ukurasa wake wa Facebook mnamo Jumatatu jioni na kukosolewa sana, mwimbaji huyo mwenye umri wa miaka 43 alizichapisha tena picha zile zile kwenye ukurasa wake wa Instagram Jumanne mchana bila kuonyesha dalili yoyote ya kujuta.

Mama huyo wa watoto watano alizidi kubainisha kuwa anajivunia sana mwili wake mzuri ambao ameuweka sawa kwa kufanya mazoezi kwenye gym.

“Unaona hili vazi, Wakenya watasema mimi niko uchi, ona kuna chupa zinapasuka tayari. Kitikisa meza kimefanya hivyo tena nchini Uswidi. Waambie siendi kwenye gym bure,” Akothee alisema.

Mwimbaji huyo aliendelea kueleza kwamba ili utumbuizaji wa msanii kwenye jukwaa uwe mzuri, ni lazima avutie masikio na macho ya mashabiki.

"Muziki ni wa macho, sauti ni ya masikio, wajifunze kati ya mavazi ya kutumbuza na mtindo wa mavazi. Ikiwa hawatakubali, waache waite polisi… Ficha watanzania wasione, wajikite kwenye madaha,” alisema.

Mwanamuziki Akothee alizua hisia mseto kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii siku ya Jumatatu jioni baada ya kuchapisha picha zake akitumbuiza mbele ya mashabiki wake jijini Stockholm, Uswidi wikendi.

Msanii huyo alishiriki na mashabiki wake mtandaoni baadhi ya picha zake akitumbuiza jukwaani katika nchi hiyo ya Ulaya, ambapo alionekana akiwa amevalia vazi jeusi lenye utata ambalo lilifunika tu sehemu ya juu ya mwili wake.

Hata kabla hata wanamtandao hawajatoa maoni yao kuhusu picha hizo, Akothee alitumia sehemu ya maelezo ya chapisho hilo kujitetea na kuweka wazi kuwa yeye si mfano wa kuigwa kwa mtu yeyote.

“Huyu Ndiye AKOTHEE MSANII. Mwimbaji, mburudishaji na sio aina yako ya mfano. Msanii huyu Akothee ana soko lengwa tofauti leo. Weka mdomo wako mahali pesa zako zilipo. Akiwa na Dj Ike anayetafutwa zaidi. SWEEEEEDEN ilikuwa MOTO. Asante sana. HATUA NYINGINE,” Akothee alisema chini ya picha hizo.

Katika picha hizo, mama huyo wa watoto watano alionekana akiwapa mashabiki wake shoo ya kusisimua kwa huku wanadensi wa kike wakicheza nyuma yake.

Wanamitandao waliotoa maoni kwenye chapisho hilo walionekana kuvutiwa zaidi na vazi lake jeusi lililofunika tu sehemu yake ya juu ya mwili wake. Ukaguzi wa karibu wa picha hizo hata hivyo unaonyesha kuwa miguu na mapaja yake, licha ya kuwa yalionekana, yalifunikwa na nguo nyepesi.

Baadhi ya Wakenya ambao walitoa maoni yao walionekana kutoridhishwa na vazi la mwimbaji huyo na kwa hilo wakamshambulia huku wengine wakionekana kumtetea wakisema pia wanariadha na watu wengine mashuhuri wa kimataifa huwa wanaburudisha wakiwa wamevalia mavazi yasiyofunika mwili wote na huwa hawahukumiwi.