Kijana aozeshwa mke katika harusi ya kitamaduni na alipa mahari ya Ksh. 176 - Video

Kijana huyo aliketi kwenye mkeka akiwa ameinamisha kichwa kwa kukata tamaa ya kufunga harusi wakati waumini walipojitolea kumchangishia kiasi hicho cha pesa kulipia mahari.

Muhtasari

• Kisha walikuwa wanazungumza kuhusu ndoa hiyo lakini wakabaini kwamba kizingiti kikubwa kilikuwa mahari na ndipo walianzisha mchango.

• Mama mmoja alijitolea na kusema kwamba alikuwa radhi kumtolea shilingi elfu mbili ambazo aliingia mfukoni na kuzitoa na kuzirusha kwenye baraza hilo.

Kijana achangishiwa kufanya harusi ya kitamaduni.
Kijana achangishiwa kufanya harusi ya kitamaduni.
Image: Screengrab

Dini ya Kiislamu inajulikana na wengi kama dini ya wote, dini ambayo hushiriki mambo mengi kwa pamoja tena katika hali ya kusaidiana kubebeana mzigo.

Ndio hali iliyotokea uswahilini baada ya kijana mmoja ambaye hajatambulika jina kuchangishiwa pesa shilingi elfu tatu za Tanzania [Shilingi 176 za Kenya] ili kumuoa binti mmoja.

Katika msururu wa video ambazo zimeibuliwa kutoka katika tukio hilo la kumpendeza Mwenyezi Mungu, kijana huyo mwenye umri wa makamo alifanyiwa ndoa ya kitamaduni – ile ya Waislamu kuketi mkekani.

Tukio linaanza kijana huyo akiwa ameketi kwenye mkeka huku ubani ukiwa unatoa moshi taratibu mbele yake na amezungukwa na watu waliokuwa wamevaa majoho ya Kiislamu, kama masheikh vile.

Kisha walikuwa wanazungumza kuhusu ndoa hiyo lakini wakabaini kwamba kizingiti kikubwa kilikuwa mahari na ndipo walianzisha mchango.

Mama mmoja alijitolea na kusema kwamba alikuwa radhi kumtolea shilingi elfu mbili ambazo aliingia mfukoni na kuzitoa na kuzirusha kwenye baraza hilo.

Sheikh pia aliongeza na kijana huyo moja kwa moja akenda kulipa hiyo mahari.

Katika sehemu ya pili ya video hiyo, kijana huyo anaonekana akisindikizwa na kina mama wa Kiislamu kwenda katika nyumba ambaye mwali wake – bibi harusi mtarajiwa – alikokuwa amefungiwa ndani baada ya kufundwa.

Kijana aliingia akisindikizwa kwa nyimbo za nikkah na kumpata mpenzi wake ameketi kwa kitanda huku amefunikwa usoni.

Aliambiwa kuwa taratibu kumfunua shuka usoni na akaona ni yeye, tabasamu likatanda katika panda la uso wake.

Aliketi kando yake na wakati alitaka kuonesha haraka ya kuondoka na mkewe, kina mama waliokuwa wanashangilia kitendo hicho cha kheir walimwambia kupunguza papara kwani tayari dereva wa daladala la kuwasafirisha hadi kwao alikuwa ameridhia kusubiri wala hakuwa na haraka.

Hebu tazama video hizi hapa chini;