•Kulingana na ufichuzi wake, mwimbaji huyo amemshinda umri mumewe Denis Schweizer kwa takriban muongo mmoja kwani alizaliwa mwaka wa 1988.
•Aliwasuta wanaotumia njia tofauti kukiri hisia zao kwake, k.m. kutengeneza mabango na akawakosoa vikali wanaofanya hivyo.
Mwimbaji na mjasiriamali mashuhuri Esther Akoth almaarufu Akothee amepinga vikali madai kwamba mume wake Denis ‘Omosh’ Schweizer ni Mpakistani.
Siku ya Jumatano asubuhi, msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alionyesha kitambulisho cha mzungu huyo kuthibitisha kuwa yeye ni Mswizi.
Mama huyo wa watoto watano alidokeza kwamba Bw Schweizer alizaliwa na kukulia mjini Bern, Uswizi ambako wanafamilia wake wengine pia wanaishi. Pia alifichua kuwa mzungu huyo ana umri wa takriban miaka 35.
“DENIS EDUARD SCHWEIZER alizaliwa na kukulia Uswisi, Bern mwaka wa 1988. Pakistan ni wewe na njaa ya kwenu . Mama yake na familia yake wanaishi Uswizi,” Akothee alisema siku ya Jumatano asubuhi kupitia ukurasa wake wa Facebook.
Aliendelea kufichua kuwa tayari alikuwa amekutana na wanafamilia wa Omosh katika siku za nyuma na akamsifu sana mama mkwe wake.
Mwimbaji huyo pia aliwataka Wakenya kuheshimu usiri wa maisha yake ya kibinafsi na akabainisha kuwa hatafafanua kilichotokea katika ndoa yake.
"Nimekutana na wanafamilia wake wote na mama yake ni single mother mrembo na mzuri sana. Nilimuita mume wangu Bw Omosh ili kumlinda dhidi ya uhasi mtandaoni kabla ya kumtambulisha mtandaoni. Sasa kwa vile hayupo mtandaoni tena nyie mmepika vitu vyenu, akaenda akafuta akaunti zake za mitandao ya kijamii. Ninawaomba muchane na maisha yangu ya kibinafsi. Ndoa yangu iko Off line na haitatokea popote si kwenye mahojiano wala kutajwa kwa kuwa hamstahili ufafanuzi wa kilichotokea wapi,” alisema.
Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 pia alionyesha kutoridhika kwake na wanaume wanaotumia njia tofauti kukiri hisia zao kwake, k.m. kutengeneza mabango na akawakosoa vikali wanaofanya hivyo.
"Jambo hili la Pakistani limewafanya chokoras wafikirie Akothee ni Mistry. Nilikutana na Omosh Uswizi, kwa hiyo pata kazi kwanza kabla ya kupachika hizo kadi zisizo na maana, nataka kumuoa Akothee, unataka kumuoa na nini chako? Unataka kuolewa na Akothee au unataka kulelewa na AKOTHEE. Hiyo ni Njaa,” Akothee alisema.
Aidha, aliwataka watu kutofautisha maisha yake ya kibinafsi na chapa ya Akothee akibainisha kwamba alijijengea jina hilo kutokana na ujasiri, uaminifu, nidhamu na bidii.