Ex wa Diamond, Zari Hassan azungumza kuhusu kujuta kumpoteza mpenzi

Zari ameweka wazi kuwa hakuna mtu mwenye mamlaka ya kumwambia kuwa atajuta uhusiano wao kuvunjika.

Muhtasari

•Zari Hassan amebainisha kuwa pesa anazofanyia bidii sana kutafuta ndicho kitu pekee ambacho angejutia kupoteza.

•Alionekana kutuma ujumbe kwa watu ambao uhusiano wake nao umetatizika au wale ambao watakosana naye siku za usoni.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Mwanasholaiti maarufu wa Uganda, Zari Hassan, ameweka wazi kuwa hakuna mtu yeyote mwenye mamlaka ya kumwambia kuwa atajuta uhusiano wao kuvunjika.

Jumatatu asubuhi, mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 43 ambaye kwa sasa anaishi Afrika Kusini alichapisha video yake akionekana kwenda kazini.

Kwenye video hiyo, mama huyo wa watoto watano alibainisha kuwa pesa anazofanyia bidii sana kutafuta ndicho kitu pekee ambacho angejutia kupoteza.

“Pesa pekee ndiyo yenye haki ya kuniambia, ‘utajuta kunipoteza.’ Wengine wanaweza kutulia,” aliandika Zari kwenye video hiyo.

Kuna uwezekano mkubwa kuwa mzazi mwenza huyo wa staa wa bongo Diamond Platnumz alikuwa akituma ujumbe kwa watu ambao uhusiano wake nao umetatizika au wale ambao watakosana naye siku za usoni. Huenda alikuwa akiwahutubia wapenzi au watu wa karibu.

Image: INSTAGRAM// ZARI HASSAN

Kwa sasa Zari ameolewa na mfanyabiashara wa Uganda, Shakib Cham Lutaaya ambaye alifunga naye ndoa rasmi mapema mwezi huu nchini Afrika Kusini.

Wanandoa hao walirasimisha walifanya harusi ya faragha jijini Pretoria, Afrika Kusini mnamo Oktoba 3 baada ya kuchumbiana kwa zaidi ya mwaka mmoja. Maelezo ya harusi hiyo yalikuwa yamefichwa sana lakini tulifanikiwa kupata baadhi ya picha na video za sherehe hiyo ya kukata na shoka.

Picha hizo zilionyesha  Zari akiwa amevalia gauni la harusi refu jeupe huku mumewe Shakib akiwa amevalia suti ya kijivu na shati jeupe.

Wanafamilia wakiwemo watoto wa Zari; ; Pinto Tale, George Ssemwanga, Dido Ssemwanga Tiffah Dangote na Prince Nillan walikuwepo kwenye hafla hiyo. Tiffah alivalia gauni jeupe huku Nillan akiwa amevalia suti ya kijivu na shati jeupe sawa na bi na bwana harusi.

Wana wa Zari na aliyekuwa mume wake, Ivan Ssemwanga walionekana wamevalia suti nyeupe, shati jeupe na viatu vyeupe.

Wengi wa wageni waliokuwa wamealikwa kuhudhuria hafla hiyo ya faragha walionekana wamevaa mavazi meupe. Wanaume walikuwa na suti ya kijivu wakati wanawake walivaa gauni za rangi ya dhahabu.

Video inamuonyesha Shakib akisema viapo vya ndoa kisha kumvisha Zari pete kidoleni kabla ya wageni kupiga makofi kwa nguvu. Video nyingine inawaonyesha wanandoa hao wakiwa na watoto wa Zari wakipigwa picha ya familia huku wageni wakipiga makofi.

Mama yake Shakib pia alikuwepo kwenye sherehe hiyo.

Wawili hao walihalalisha muungano wao wa muda mrefu kwa mara ya kwanza katika harusi ya kidini ya Kiislamu (Nikah) mapema mwaka huu.