Mpenzi wa Mungai Eve, Director Trevor hatimaye afichua mipango ya mahari na harusi

Mwelekezaji huyo alidai kwamba anapanga kutoa mahari ya takriban shilingi milioni kumi hadi milioni kumi na tano.

Muhtasari

•Director Trevor alisema bado anakusanya pesa za kutosha kabla ya kuchukua hatua ya kufanya mazungumzo na familia ya Eve.

•Kuhusu mipango ya ndoa, alisema wataufanya muungano wao kuwa rasmi baada ya yeye kutoa mahari yote.

Image: INSTAGRAM// MUNGAI EVE

Director Trevor, mpenzi wa Mungai Eve amezungumza kuhusu mipango yake ya kufunga ndoa rasmi na mtayarishaji maudhui huyo mashuhuri wa Kenya.

Katika mahojiano ya simu na kituo kimoja cha redio cha humu nchini, muelekezaji huyo wa video ambaye jina lake halisi ni Bonventure Monyancha alifichua kuwa tayari amemtambulisha Eve kwa familia yake.

“Shemeji ashafika nyumbani. Kila kitu pale ishafanywa,” Director Trevor alisema.

Hata hivyo alikiri kuwa bado hajalipa mahari kwa familia ya mrembo huyo mwenye umri wa miaka 23.

Huku akielezea kwa nini bado hajapiga hatua hiyo, Trevor alisema kuwa bado anakusanya pesa za kutosha kabla ya kuchukua hatua ya kufanya mazungumzo na familia ya Eve.

“Bado, bado natafuta hela, unajua yule hela zake ni kama mamilioni hivi,” alisema.

Mwelekezaji huyo alifichua kuwa anapanga kutoa mahari ya takriban shilingi milioni kumi hadi milioni kumi na tano za Kenya.

“Unajua yule kila mwaka mahari inapanda. Nitalipa kama milioni 10-15. Ikifika miaka miwili kutoka sasa itakuwa imefika kama 15,” alisema.

Pia aliweka wazi kuwa tayari ameshaamua kutulia na mtayarishaji wa maudhui huyo mwenye umri wa miaka 23 akieleza kuwa yeye ndiye pekee ambaye moyo wake unamtaka.

Kuhusu mipango ya ndoa, alisema wataufanya muungano wao kuwa rasmi baada ya yeye kutoa mahari yote.

"Harusi ni baada ya kulipa mahari," alisema.

Director Trevor na Mungai Eve waliadhimisha miaka mitano ya kuwa pamoja mapema mwaka huu.

Alipokuwa akisherehekea hatua hiyo muhimu mwezi Januari, Eve alimwandikia mpenzi wake ujumbe mtamu akionyesha shukrani zake kwa mapenzi yao,  kuanzia mwanzo wao mnyenyekevu hadi hadhi yao ya sasa kama wapenzi wanaojikimu.

“Asante kwa kuwa baraka katika maisha yangu na kunipa urafiki ambao nimekuwa nikihitaji maisha yangu yote,” Eve aliandika.

Eve pia alimsherehekea Trevor kwa kumsukuma katika kazi yake ya sasa, ambapo sasa wanakusanya pesa nyingi.

"Tumekuwa na misukosuko yetu lakini tumestahimili mtihani wa wakati, ninaombea upendo ambao hudumu maisha yote na urafiki usio na mwisho.Siku zote namshukuru Mungu kwa kukuleta katika maisha yangu, wewe ni baraka na mafanikio yangu bora zaidi, asante kwa kunisapoti kila wakati, kuniamini, na kunisukuma kwa bidii kuwa toleo bora zaidi kwangu. nakupenda leo na hata milele," aliandika.