Georgina Njenga azungumzia kuingia kwenye mahusiano mengine baada ya kutengana na Baha

Georgina alithibitisha kutengana na Baha mwezi Julai, mwaka jana.

Muhtasari

•Mama huyo wa binti mmoja alibainisha kuwa kuingia katika uhusiano mwingine sio kipaumbele chake kwa sasa.

•Katika mahojiano na Mungai Eve mwezi Agosti,  alisema kuwa uhusiano wao ulikuwa na matatizo hata kabla ya wote wawili kuamua kutengana.

wakati wa mahusiano yao.
Georgina Njenga na Baha wakati wa mahusiano yao.
Image: INSTAGRAM// GEORGINA NJENGA

Mtayarishaji wa maudhui wa Kenya Georgina Njeri Njenga amejibu kuhusu iwapo anapanga kuingia katika mahusiano mengine hivi karibuni.

Maisha ya mapenzi ya Georgina yamebaki kuwa siri tangu alipothibitisha kuachana na mwigizaji Tyler Mbaya, maarufu kama Baha, katikati ya mwaka jana.

Wakati akiwashirikisha mashabiki wake katika kipindi cha maswali na majibu kwenye mtandao wa Instagram siku ya Ijumaa jioni, mfuasi mmoja alimuuliza kuhusu mipango yake ya uchumba.

“Utachumbiana hivi karibuni?” shabiki aliuliza.

Katika majibu yake, mama huyo wa binti mmoja alibainisha kuwa kuingia katika uhusiano mwingine sio kipaumbele chake kwa sasa.

“Na hii story huwasumbua. Anyway sio kipaumbele katika maisha yangu kwa sasa,” Georgina alijibu.

Haya yanajiri takriban miezi sita tangu mrembo huyo mwenye umri wa miaka 23 athibitishe kuachana na baba wa bintiye wa pekee, mwigizaji Tyler Kamau Mbaya.

Georgina alifunguka kuhusu kutengana na Baha mwezi Julai mwaka jana na kudai kuwa tayari alikuwa kwenye uhusiano mwingine wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu kwenye Instagram.

Shabiki aliuliza ikiwa wapenzi bado walikuwa pamoja.

"Hapana, tuliachana," alijibu.

Aliongeza, "Wengi wenu mnauliza swali hili. Hii ni mara ya mwisho kujibu. Tuliachana. Niko kwenye uhusiano mpya na mtu wangu mpya!" .. "Hii ni aina tofauti ya mapenzi! Kwa kweli sikujua kwamba upendo kama huo ulikuwepo hapo awali, niko mahali pazuri.

Katika mahojiano na Mungai Eve mwezi Agosti, mama huyo wa binti mmoja alisema kuwa uhusiano wao ulikuwa na matatizo hata kabla ya wote wawili kuamua kutengana.

"Hakukuwa na sababu maalum kwa nini tuliachana. Masuala yalirundikana, hakukuwa na masuala mahususi, yalikuwa ni makubaliano ya pande zote kuwa haya hayafanyiki. Hakuna aliyemuacha mwingine, tulikaa chini na kuhisi hii imeenda, tulijaribu kuzungumza kwa muda mrefu lakini... Tulijaribu kuhusisha kupitia familia.” Georgina alisema.

 Alisema kuwa kwa sababu tu alikuwa na mtoto na Baha, hiyo haikuwa tosha kwa yeye kusalia kwenye uhusiano huo.

"Mtoto isiwe sababu ya kukaa kwenye uhusiano, unaweza kuwa mzazi mwenza. Tyler anampenda binti yake na yuko katika maisha yake. Nilijua kuwa atakuwa huko hata nilipokuwa mjamzito." alisema.