Hongera! Nyota Ndogo ajaliwa mtoto na mumewe mzungu, azua wasiwasi kuhusu rangi yake

Mwimbaji huyo alielezea wasiwasi wake kuhusu sura ya mwanawe akidai kuwa hafanani na mzazi mwenzake.

Muhtasari

•Nyota Ndogo alichapisha picha ya mtoto mchanga kwenye kurasa zake mtandao wa kijamii na kumtaja kama mrithi wake.

•Mtoto mchanga wa mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 ni wake wa kwanza na mume wake mzungu, Bw Henning Neilsen.

Image: INSTAGRAM// NYOTA NDOGO

Wikendi, mwimbaji mkongwe wa Kenya Mwanaisha Abdalla almaarufu Nyota Ndogo alitangaza kuzaliwa kwa mtoto wake wa tatu.

Huku akishiriki habari hizo nzuri na mashabiki wake, Nyota Ndogo alichapisha picha ya mtoto mchanga kwenye kurasa zake mtandao wa kijamii na kumtaja kama mrithi wake.

Mwimbaji huyo hata hivyo alielezea wasiwasi wake kuhusu sura ya mtoto huyo wake akidai kuwa hafanani na mzazi mwenzake.

"Karibu nyumbani mwanangu, ila hii rangi sinitaambiwa nimechiti, yani umeamua nywele ndio uchukue ya baba rangi ndio hii yetu, karibu abdalla.(URITHI TUNAO)."

Mtoto mchanga wa mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 43 ni wake wa kwanza na mume wake mzungu, Bw Henning Neilsen.

Mwimbaji Nyota Ndogo alitangaza habari za ujauzito wa ambaye atakuwa mtoto wake wa tatu mapema mwezi Septemba  mwaka jana kutumia picha ambayo  ilimuonyesha akiwa ameshika tumbo lake lililoonekana kuchomoza.

Baadaye, mama huyo wa watoto watatu hata hivyo aliweka wazi kuwa mume wake, Henning Neilsen amemuonya dhidi ya kuzungumza mengi kuhusu ujauzito wake na vyombo vya habari au watu wengine wa nje.

Msanii huyo mwenye umri wa miaka 42 ambaye kwa sasa anaendesha mkahawa wake katika eneo la VoI alisema ameruhusiwa tu kujizungumzia yeye na muziki wake na sio ujauzito hadi atakapojifungua.

“Asanteni kwa hongera zenu, lakini media mtanisamehe mume wangu amesema hataki kuona kwenye kituo chochote cha radio TV ama polisi nikiongelea hali yangu. Kwa hiyo endapo nitatoa interview iwe ya mimi na mziki wangu na sio ujauzito wangu, ama nisitoe mpaka nijifungue,” Nyota Ndogo alisema.

Baadaye mwezi huo, Nyota Ndogo alifichua kwamba mume wake mzungu alikuwa amemnunulia shamba lenye thamani ya shilingi milioni tatu ambapo anakusudia kujenga hoteli kubwa zaidi ya anayoendesha kwa sasa.

"Nimekua nikiona jumbe nyingi kuhusu hoteli yangu kua niko kibandani mara hapa sio hadhi yako na wengine hata kunifanani na kina shishi kinaa @esha.s.buheti ambao ndio watu ninao waangali na kufata nyayo zao. Lakini ni miaka sita sasa pale hotelini na sijakua na haraka yakufanya kitu ama kujipa presha kwaku wenzangu wapo vizuri hapana, naendaga na time, na time ndio saa," alisema Nyota Ndogo.

Mwimbaji huyo wa kibao 'Watu Na Viatu' ana watoto wengine wawili.