logo

NOW ON AIR

Listen in Live

Bahati afunguka kwa nini alikumbwa na stress baada ya kushindwa katika uchaguzi wa Mathare

“Sitaki kudanganya. Nilipotea miezi miwili kwa sababu ya msongo wa mawazo,” Bahati alisema.

image
na Radio Jambo

Dakia-udaku07 June 2024 - 06:50

Muhtasari


•Bahati aliwania kiti cha mbunge wa Mathare kwa tikiti ya Jubilee na kuibuka nambari tatu nyuma ya mshindi Anthony Oluoch wa ODM na Billian Ojiwa wa UDA.

•Alimshukuru naibu wa rais kwa jinsi walivyomkubali katika chama chao baada ya uchaguzi, ingawa aliwania kwa tikiti ya Jubilee.

Mwimbaji mashuhuri wa Kenya Kelvin Kioko almaarufu Bahati amekiri kuzama katika msongo wa mawazo baada ya kushindwa katika uchaguzi mkuu wa 2022.

Mwimbaji huyo wa zamani wa nyimbo za injili aliwania kiti cha mbunge wa Mathare kwa tikiti ya Jubilee na kuibuka nambari tatu nyuma ya mshindi Anthony Oluoch wa ODM na Billian Ojiwa wa UDA.

Akizungumza wakati wa hafla ya kuzindua kipindi chake cha Reality Show ‘The Bahati’s Empire’, mwimbaji huyo alikiri alitoweka kwa miezi miwili baada ya matokeo ambayo hakuyatarajia.

“Sitaki kudanganya. Nilipotea miezi miwili kwa sababu ya msongo wa mawazo,” Bahati alisema.

Aliongeza, “Unajua sikuwa nimezoea kuanguka. Nimezoea nafanya Groove Awards, nashinda watu. Sasa hii mheshimiwa nikapatana na watu ambao sijazoea kushindana nao. Kampeni inaingia natolewa mbio mheshimiwa.”

Mwimbaji huyo wa nyimbo za mapenzi alikiri hayo alipokuwa akimhutubia naibu rais Rigathi Gachagua kuhusu taaluma yake ya muda mfupi ya kisiasa. DP alikuwa mgeni wa heshima katika hafla ya uzinduzi wa Reality Show iliyofanyika katika Hoteli ya Westwood jijini Nairobi Alhamisi usiku.

Aliendelea kumshukuru naibu wa rais kwa jinsi walivyomkubali katika chama chao baada ya uchaguzi, ingawa aliwania kwa tikiti ya Jubilee.

"Nataka kukushukuru kwa kunikumbatia hata kama nilikuwa upande mwingine," alisema.

Katika uchaguzi wa Ubunge wa Mathare wa mwaka wa 2022, Oluoch wa chama cha ODM alihifadhi kiti hicho kwa kupata kura 28,098 huku Ojiwa wa UDA akiibuka wa pili kwa kura 16,912. Bahati alifanikiwa kupata kura 8,166 kwa tikiti ya chama cha Jubilee.

Mwaka jana, mwimbaji huyo mashuhuri wa nyimbo za mapenzi alijiunga rasmi na chama tawala cha UDA.

Bahati alikaribishwa kwenye chama cha UDA  na katibu mkuu wa chama hicho Cleophas Malala.

Katika taarifa yake baada ya kupiga hatua hiyo, aliweka wazi kwamba alifurahi kupiga hatua hiyo kubwa ya kisiasa.

"MWANA MPOTEVU 🙏 NINA FURAHA KURUDI NYUMBANI. NIMEPOKELEWA RASMI NA KATIBU MKUU WA CHAMA CHA U.D.A MHE. CLEOPAS MALALA, VIONGOZI WENGINE NA WANAMUZIKI WENZANGU KATIKA  MAKAO MAKUU," alisema.

Mwanamuziki huyo mwenye umri wa miaka 30 alimshukuru kiongozi wa chama cha UDA, rais William Ruto kwa kile alichosema, ameweka mazingira mazuri kwa vijana kujiendeleza humu nchini.

Wakati huo huo, alidokeza kwamba atawania kiti cha ubunge wa Mathare kwa tiketi ya chama hicho ifikapo 2027.


RADIO JAMBO FREQUENCIES

Kisumu 100.1 | Mombasa 92.3 | Nakuru 96.9 | Eldoret 99.5 | Nyeri 99.3 | Nyahururu 97.3 | Webuye 95.3 | Meru 92.7 | Kitui 104.9 | Kibwezi 104.7 | Voi 105.7 | Malindi 98.1 | Lamu 104.7 | Narok 97.3 | Kapenguria 99.7 | Kisii 89.3 | Garissa 104.3 | Maralal 97.3 | Lodwar 92.7


logo© Radio Jambo 2024. All rights reserved