Rayvanny amsifia mkewe kwa kusimama naye licha ya changamoto nyingi za mahusiano

Rayvanny alibainisha kuwa tayari walikuwa wamepitia changamoto nyingi katika uhusiano wao.

Muhtasari

•Rayvanny alitambua urembo wa mama huyo ya mwanawe na kumthamini kwa kumchagua yeye badala ya wanaume wengine wote.

•Wakati akimjibu baba huyo wa mtoto wake, Fahyma pia alithibitisha kumpenda sana mwimbaji huyo na kuahidi kuendelea kumpenda.

Image: INSTAGRAM// FAHYMA

Mwimbaji mashuhuri wa Bongo Fleva Raymond Mwakyusa almaarufu Rayvanny amemsherehekea mke wake mrembo Fahyma huku akiadhimisha siku yake ya kuzaliwa.

Katika ujumbe mzuri aliomwandikia mpenziwe kwenye mtandao wa Instagram, bosi huyo wa lebo ya Next Level Music alitambua urembo wa mama huyo ya mwanawe na kumthamini kwa kumchagua yeye badala ya wanaume wengine wote.

Rayvanny alibainisha kuwa tayari walikuwa wamepitia changamoto nyingi katika uhusiano wao lakini akashukuru kuwa Fahyma ameendelea kusimama naye.

“Sura yako na uzuri ulionao ungeweza kwenda kwa yoyote ile ukanichagua mimi, Mengi tumepitia lakini bado upo upande wangu ❤️‍🔥,” Rayvanny aliandika.

Msanii huyo wa zamani wa WCB  aliambatanisha ujumbe wake na picha ya mkewe mrembo na kuendelea kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa.

“Wewe sio tu Mwanamke ila ni Mama !!! Mama Ake Chui @fahyvanny 🐆 NAKUPENDA SANA !!! Happy birthday maisha yangu!!! Enjoy Your Day,” aliandika.

Wakati akimjibu baba huyo wa mtoto wake, Fahyma pia alithibitisha kumpenda sana mwimbaji huyo na kuahidi kuendelea kumpenda.

“Nakupenda sana mume wangu na nitakupenda leo, kesho mpaka milele,” alijibu.

Fahyma ambaye pia anatambulika kama Fayvanny na mzazi mwenzake, Rayvanny wamekuwa wakionyesha mapenzi mazito baina yao tangu warudiane mapema mwaka jana baada ya awali kutengana takriban miaka mitatu iliyopita.

Mwezi Aprili mwaka jana, Rayvanny alidhihirisha mapenzi yake kwa mzazi huyo mwenzake kwa kuchorwa jina lake kwenye kifundo cha mkono wake.

"Fahyma...❤," ilisomeka tattoo mpya ya mwimbaji huyo.

Bosi huyo wa Next Level Music alionyesha video yake akichorwa katika duka moja la tattoo jijini Arusha, Tanzania na akaweka wazi alichukua hatua hiyo kutokana na mapenzi yake makubwa kwa mzazi huyo mwenzake.

Alisema, licha ya kuwa ni chungu, alilazimika kufanya hivyo kutokana na athari kubwa ya Fahyma katika maisha yake.

"Inauma sana ila nimefanya hivi kwa ajili yako Fahvanny," alisema kwenye ukurasa wake wa mtandao wa Instagram.

Aliongeza, "Umekuwa mwanamke wa tofauti kwangu, nakuheshimu."

Alibainisha kwamba iwapo watu wangeelewa mapenzi yake kwa mwanamitindo huyo basi wangeelewa hatua hiyo yake.

"Hata ungekuwa wewe ungechora tu," alisema.