Jamaa mmoja amewashangaza wakenya baada ya kusimulia jambo ambalo mpenzi wake wa zamani aliwahi kumfanyia na ambalo hatolisahau kamwe.
Akizungumza kwenye runinga ya TV47 katika kipindi kinachoongozwa na mchekeshaji Dr Ofweneke, jamaa huyo ambaye alikuwa mmoja wa hadhira kwenye kipindi hicho alisema kwamba walikuwa wanaishi na mpenzi wake jijini Nairobi kabla ya kukosana.
Pia aliweka wazi kwamba wazazi wake nyumbani, kaunti ya Siaya walikuwa wanamfahamu mrembo huyo.
Wakati mmoja baada ya kukosana ghafla, mrembo huyo alifunga safari kinyemela kwenda nyumbani kwa kina mume.
Alifika akakaribishwa vizuri, kumbe lengo lake lilikuwa kumuibia mama mkwe simu kama njia moja ya kumuadhibu mume wake kwa kumuacha.
“Huwa inaniuma lakini itabidi niseme, nilikuwa na mrembo na tuliachana tu kwa njia rahisi, lakini yeye huwezi amini alitafuta nauli akaenda hadi kijijini kwetu Siaya. Akahakikisha amechukua simu ya mamangu akarudi nayo Nairobi,” mwanamume huyo alisimulia.
“Unajua mama hakuwa anajua kama tumeachana, akafika na akakaribishwa kwa chai wakazungumza kidogo na mama akatoka kidogo kuenda kutafutia ng’ombe nyasi, kurudi akapata simu imeibwa,” aliongeza.
Simulizi ya bwana huyu iliwatoa wengi pangoni na kufungua roho kuhusu matukio waliyopigwa na wapenzi wao baada ya kuachana ghafla.