Raia wa Nigeria, Oside Oluwole, anayejulikana kwa jina la "Khoded," amevunja rekodi ya dunia kwa kucheza mchezo wa video wa kandanda ,'dream league soccer 2023' kwa takriban masaa 75.
Utendaji wa ajabu wa Oside kwenye mchezo wa video ulizidi kwa mbali rekodi ya awali ya saa 50, iliyowekwa na mwingereza David Whitefoot mnamo 2022.
Katika mabadiliko ya kipekee, Oside alichagua kucheza mchezo huo kwenye simu yake aina ya iPhone,iliyounganishwa kwenye skrini ya runinga, tofauti na waliokuwa na rekodi za awali ambao walipendelea FIFA au 'Pro Evolution Soccer'.
Katika masaa hayo (masaa 75) Oluwole alicheza mechi zaidi ya 500 huku akifurahia tangu kuanza kucheza mwaka wa 2016.
Kulingana na mwongozo wa rekodi za dunia za Guinness , Oside aliruhusiwa kupumzika kwa dakika tano kwa kila saa ya mchezo. Mapumziko haya yalikuwa fursa zake pekee za kula, kulala au kutumia choo.
Akitafakari tukio hilo, alisema:
“Nilifurahia sana kucheza kwa muda wa saa 75 moja kwa moja na saa chache tu za kupumzika. Haikuwa kazi rahisi, lakini lazima niseme ilikuwa ya kufurahisha. Ilikuwa ni wakati mzuri sana; tukio hilo lilikuwa la kuvutia sana na ninamshukuru Mungu kwamba lilifanikiwa.”
Rekodi hiyo, ambayo awali iliwekwa saa 24 mnamo 2010, iliongezeka polepole hadi saa 50 katika kipindi cha miaka 11 kabla ya utendakazi wa Oside.