Msanii na mjasiriamali mashuhuri wa Kenya Esther Akoth almaarufu Akothee amesherehekea mambo makubwa aliyofanikisha kufanya katika miaka yake ya 30.
Katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa watoto watano alifichua kuwa akiwa na umri wa miaka 31, tayari alikuwa amejijengea nyumba, akajengea wazazi wake na nyanyake.
Pia alibainisha kuwa wakati huo tayari alikuwa akiwalea watoto wake peke yake, akiendesha biashara na kufanya safari za kimataifa.
“HUYU NDIYE MADAMBOSS, nilifanya hivi miaka 11 iliyopita. Ulikuwa wapi miaka 11 iliyopita? Nilikuwa na umri wa miaka 31, tayari nilikuwa nimejenga nyumba yangu ya kustaafu, nimewajengea wazazi wangu nyumba mpya kabisa nikawanunulia magari mawili mapya kabisa, nikamjengea bibi yangu nyumba,” Akothee aliandika siku ya Ijumaa asubuhi chini ya picha ya nyumba yake, nyumba ya mzazi wake na ile ya nyanya yake.
Aliongeza, “Mbali na kulea watoto wangu peke yangu, nilikuwa nikiwasaidia ndugu zangu, nikiendesha biashara zangu, nikihama kutoka mahakama moja hadi nyingine nikipigana vita vya baba za watoto wangu, kusafiri kwa ndege katika eneo la biashara, ndege za kibinafsi na mengine, kujenga taaluma yangu, kutafuta elimu yangu, na kung;aa na kuishi kwa usawa.”
Msanii huyo mwenye umri wa miaka 43 alibainisha kuwa sasa amepata mengi na amepata usawa wa maisha na amani.
“Sasa nimepata usawa na amani. Nilifanya yote niliyotaka kufanya katika miaka yangu ya 30 sasa ninafurahia maisha yangu katika miaka yangu ya 40 na kusawazisha cheki zangu & kujitunza wazazi wangu na biashara zangu, kurudisha kwa jamii na kujenga urithi💪," alisema.
Aliongeza, “Sasa ninapata mapenzi, kuachwa na kuachana pia na tunasonga mbele 🤣🤣🤣 shoneni vitenge bibi harusi bado yuko fiti."
Akothee pia alibainisha kuwa watoto wake wote wanafanya kazi na wako thabiti, jambo ambalo anajivunia sana.