Mpenzi wa Mulamwah, Ruth amekanusha madai ya ‘kumpokonya’ mchekeshaji huyo kutoka kwa aliyekuwa mpenzi wake, Caroline Muthoni almaarufu Carrol Sonie.
Wakati akiongea kwenye video iliyochapishwa kwenye chaneli yake ya YouTube, mama huyo wa mtoto mmoja alibainisha kuwa madai hayo yalianza wakati yeye na Mulamah walipoamua kutangaza uhusiano wao kwenye mitandao ya kijamii.
Ruth Alikanusha kumuiba baba huyo wa mtoto wake kutoka kwa Sonie, na kuwataka watumiaji wa mtandao kukoma kuhitimisha mambo kabla ya kupata ukweli.
“Kulingana na vile mimi najua mambo iko kwa ground, sio kulingana na vile nyinyi mnasema mitandaoni. Mulamwah alikuwa ananiambia mambo itakuwa sawa kadri muda unavyosonga, ananiambia nitulie. Tukapita kipindi hicho, lakini hadi wa leo, kuna watu wananiita mume mnyakuzi,” Ruth alisema.
Mrembo huyo alibainisha kuwa Mulamwah alimsaidia sana kukabiliana na mashambulizi hayo mtandaoni na akasema kwamba mpenzi wake ataeleza kilichotokea.
Ruth pia alizungumza kuhusu uhusiano wake na Carrol Sonie akibainisha kuwa hawajawahi kuwa marafiki na hawajawahi hata kukutana.
“Hiyo stori ya husband snatcher ilitokea vile Carol, ambaye namheshimu sana, Mama Keilah alisema Ruth ni rafiki yangu. Nadhani watu walihitimisha kuwa Carol na Ruth ni mabeshte, akachukua Baba Kalamz. Hapo ndio mambo ikawa vibaya. Watu wakachukulia vile haikufanyika. Mambo ya husband snatcher ikatokea hapo,” alisema.
Aliongeza, “Mimi na Carol hatujawahi kutana, hatukuwahi kusoma pamoja. Hatujawahi kuwa mabeshte katika hali hiyo. Sijawahi kuwa marafiki na Carrol, anaweza kuthibitisha hili. Hatujawahi kusomea shule moja. Hatujawahi kutana kwa sababu maisha yangu nimekaa Eldi, nimesomea huko, Nairobi nimekuja tu juzi. Kitale tu ndo nimeenda juzi nikipeleka Baba Kalamz, lakini hatujawahi kutana (na Carol).”
Mulamwah alimtambulisha Ruth K kwa mashabiki wake mnamo Desemba 2022, muda mfupi baada ya Carrol Sonie kutangaza kuachana naye.