Anjella apewa gari jipya na Zuchu baada ya aliyekuwa bosi wake, Harmonize kumpokonya alilompa

Baada ya kutoka Kondegang, Anjella alilalamika kuhusu Harmonize kuchukua kila kitu alichompa ikiwa ni pamoja na gari.

Muhtasari

•Siku ya Alhamisi, Agosti 22, Zuchu alitimiza ahadi yake kubwa ya kumnunulia gari  msanii huyo wa zamani wa Konde Music Worldwide.

•Wakati akiwa kwenye lebo ya Konde Music Worldwide,Anjella alikuwa amezawadiwa gari na bosi wake, Harmonize.

Anjella, Diva The Bawse, na Zuchu
Image: HISANI

Malkia wa muziki Bongo Anjella Tz ametoa shukrani zake baada ya mwimbaji mwenzake Zuhura Othman almaarufu Zuchu kumzawadia gari jipya kabisa.

Siku ya Alhamisi, Agosti 22, Zuchu alitimiza ahadi yake kubwa ya kumnunulia gari  msanii huyo wa zamani wa Konde Music Worldwide, ambayo alimpa hivi majuzi.

Anjella ambaye alieleza wazi matatizo yanayomkabili kwa kutokuwa na gari hakuweza kuficha furaha yake wakati malkia huyo wa WCB akimzawadia gari jipya aina ya Toyota Crown, kama alivyoahidi. Alizamia kwenye akaunti zake za mitandao ya kijamii kueleza furaha yake na kumshukuru Zuchu kwa ishara nzuri aliyokuwa ameonyesha.

“Napenda nafasi hii kukushukuru dada angu @officialzuchu ulichokifanya ni kikubwa sana tena sana umenipa nguvu ya kuinuka tena na umeipa faraja familia yangu wazazi nilikua napata shida sana kuhusu usafiri huu umeniipa gari nakushukuru sana dada angu,” Anjella aliandika kwenye Instagram.

Mwimbaji huyo mwenye sauti nzuri aliambatanisha taarifa yake na picha zake akipokea gari hilo jipya nyeupe Alhamisi jioni.

”Umenionesha upendo mkubwa sana, Mungu akuzidishie mafanikio zaidi na zaidi. Umenifanya nijihisi mpya katika hii dunia umenifanyia jambo kubwa sana katika kipindi ambacho sikua na tumaini lolote. Dada angu @officialzuchu nakupenda sana nakuombea mungu akupe maisha marefu na mafanikio zaidi❤️,” aliongeza.

Anjella pia alimshukuru mtangazaji wa Wasafi Media, Diva The Bawse ambaye aliwezesha mawasiliano kati yake na Zuchu wakati wa mahojiano ya moja kwa moja.

"Pia Nakushukuru sana Dada angu @divatheebawse chochote kilichotokea kimepitia kwangu maisha marefu,afya njema na mafanikio zaidi. Umeonionesha upendo kama mdogo ako umenifungulia njia mpya ya maisha asante sana dada angu @divatheebawse,” alisema.

Anjella ambaye awali alikuwa amesainiwa chini ya lebo ya muziki ya Konde Music Worldwide kabla ya kuondoka mwaka 2022 alikuwa amefunguka masaibu ya kutokuwa na gari akiwa katika mahojiano na Diva The Bawse. Wakati akiwa kwenye lebo, alikuwa amezawadiwa gari na bosi wake, Harmonize.

Baada ya kutoka katika Kondegang, Anjella alilalamika kuhusu Harmonize kuchukua kila kitu alichokuwa amempa ikiwa ni pamoja na gari alilomzawadia.