•Bi Musila alibainisha kuwa mwimbaji huyo kuwa katika maisha yao ni baraka na akamhakikishia kuhusu upendo wao mkubwa kwake.
•Mama huyo wa watoto watatu alisisitiza kauli ya ya binti yake wa pekee, Gilda Naibei kuhusu mwimbaji Guardian Angel.
Siku ya Ijumaa, mke wa msanii Guardian Angel Esther Musila alikiri jinsi yeye na familia yake wanajivunia mwimbaji huyo wa nyimbo za injili.
Katika taarifa kwenye ukurasa wake wa Instagram, mama huyo wa watoto watatu alitoa shukrani zake kwa Guardian Angel kwa kusimama naye pamoja na familia yake.
Bi Musila alibainisha kuwa mwimbaji huyo kuwa katika maisha yao ni baraka na akamhakikishia kuhusu upendo wao mkubwa kwake.
"Baba G, sisi kama familia yako, tunajivunia wewe. Asante kwa kusimama nasi, kwa kumpenda kila mmoja wetu. Tumebarikiwa kuwa na wewe katika maisha yetu, na tunakupenda.. ❤️❤️❤️,” Esther Musila aliandika.
Aliambatanisha ujumbe huo na picha nzuri zilizomuonyesha yeye, Guardian Angel na familia yao wakati wa tamasha la hivi majuzi la mwimbaji huyo wa muziki wa injili, Gospo1 lililofanyika katika hoteli ya Sankara, jijini Nairobi.
”Tunaomba kwamba Mwenyezi aendelee kukuongoza na kukulinda siku zote za maisha yako🙏🏽🙏🏽🙏🏽@onlygilda,@__jama1 @mss_shali, @fred.musila.7,” aliongeza.
Mama huyo wa watoto watatu alisisitiza kauli ya ya binti yake wa pekee, Gilda Naibei kuhusu mwimbaji Guardian Angel.
Baada ya tamasha la Gospo1, Gilda alimmwagia sifa nyingi babake wa kambo, Guardian Angel, akampongeza na kueleza jinsi anavyojivunia mwimbaji huyo wa nyimbo za injili kutokana na tukio hilo lenye mafanikio.
Alisema mume huyo wa mamake aliafikia matarajio ya mashabiki na kufanya kila mtu kufurahia tamasha hilo.
“Mwanaume huyu! Aliiua (x3), nilitamani shoo hii haiwezi kuisha sasa hivi! Kama ingendelea… Lakini, ninajivunia wewe. Ulifanya kile ambacho kila mtu alitaka kusikia,” Gilda alisema.
Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 30 alibainisha kuwa Guardian alifanya mambo mengi na kupita kawaida ili kufanikisha shoo hiyo.
"Ninajivunia yeye sana, alifanya kila kitu; alikuwa DJ, alikuwa anaimba.. Namaanisha, hii ilikuwa shoo ya kiroho, na aliweza kuwapa watu kile walitaka. Watu walikuwa wakimsifu Mungu,” alisema.
Pia alisema kuwa ilikuwa jambo nzuri kutangamana na mashabiki wa Guardian Angel na akawashukuru kwa sapoti yao.
"Ikiwa unamsapoti Guardian, tuko naye 100%. Sisi ndio ambao huwa naye kawaida na huwa tunamwambia kila siku "unaweza kufanya hivi", lakini bila nyinyi mashabiki, nyinyi ni kila kitu," alisema.
Gilda alimaliza mahojiano hayo kwa kumtambua babake wa kambo kama supastaa.