•Kijana huyo mwenye umri wa miaka 27 amekiri hana cheti cha kuzaliwa, kitambulisho wala paspoti na anahitaji usaidizi kuvipata.
•Siku hiyo hiyo, pia alitunukiwa simu ya aina ya iPhone 11 na mfanyabiashara mwingine.
Bradley Marongo almaarufu Gen-z Goliath anatafuta usaidizi wa kupata stakabadhi mbalimbali muhimu za utambulisho.
Haya ni kwa mujibu wa habari zilizotolewa na mfanyibiashara na mwanasiasa Alinur Mohamed ambaye alikuwa na mkutano naye siku ya Jumamosi.
Kulingana na Alinur, kijana huyo mwenye umri wa miaka 27 kutoka kaunti ya Vihiga hana cheti cha kuzaliwa, kitambulisho wala paspoti na anahitaji usaidizi kuvipata.
“Nilikutana na Bradley Marongo wa miaka 20. Hana kitambulisho, cheti cha kuzaliwa, wala pasipoti. Anaomba kusaidiwa kuzipata,” Alinur alisema kupitia Instagram Jumamosi jioni.
Aliambatanisha taarifa yake na picha zinazomuonyesha akiwa na mwanamume huyo mrefu ambaye amekuwa akiishi na kufanya kazi katika mtaa wa Kangemi, Nairobi.
Mfanyibiashara huyo mashuhuri pia alifichua kuwa ana mpango wa kumtafutua nyumba nzuri, kumlipia kodi ya miezi mitatu na kumnunulia nguo.
"Alinur Foundation itampatia nyumba ya chumba kimoja cha kulala, kumnunulia samani, kumlipia kodi ya miezi 3, na kumtafutia nguo na viatu," alisema.
Haya yalikuwa baadhi tu ya mambo mazuri ambayo umaarufu mkubwa wa Bradley katika wiki chache zilizopita umemletea. Siku hiyo hiyo, pia alitunukiwa simu ya aina ya iPhone 11 na mfanyabiashara mwingine.
Marongo, mwenye umri wa miaka 27, anajitambua kuwa Gen Z mrefu zaidi nchini Kenya, taji ambalo anakumbatia licha ya changamoto zinazotokana na urefu wake.
Uwepo wake mkubwa umemfanya kuwa mtu anayefahamika katika maeneo kama Kangemi, ambapo mara nyingi hutumia wakati wake kubarizi ingawa hapo awali alikuwa akiishi Kayole.
Urefu wake hata ulimfanya kuwa kivutio wakati wa maandamano ya kupinga serikali, ambapo alivutia macho ya polisi.
Anajulikana mtandaoni kama "Goliath Gen Z," Marongo ana uzito wa kilo 135 na amejikusanyia wafuasi wa 15,000 kwenye TikTok, ambapo urefu na miguu yake mikubwa inaendelea kuwavutia mashabiki wake. Jina lake kwenye mtandao wa kijamii linasomeka kwa fahari, "BRADLEY Tallest in 254."
Walakini, urefu wa Marongo pia huleta umakini usiohitajika na wakati mwingine dhihaka. Alishiriki kwamba watoto mara nyingi humwangalia kwa mshangao, na watu wengine hupiga picha bila idhini yake.
Kitanda chake kimetengenezwa kidesturi, lakini bado hawezi kujinyoosha kikamilifu. Linapokuja suala la mavazi, yeye hupendelea mashati na kaptula kubwa, kwani kupata suruali inayomkaa ni changamoto.
Kuhusu viatu, mara nyingi yeye hukimbilia kwenye masoko ya mitumba, ingawa kutazama anakovutia wakati wa ununuzi kunaweza kumkosesha raha.