Carrol Sonie afichua kwa nini alikumbwa na msongo wa mawazo hadi kuenda therapy miezi 3

Sonie alifichua kuwa mambo aliyokuwa akipitia kufuatia kutengana na mchekeshaji Mulamwah yalimuathiri sana hadi akakaribia kurukwa na akili.

Muhtasari

•Sonie amesisitiza alichukua mapumziko kutoka kwa kuunda maudhui kutokana na masuala ya kisaikolojia aliyokuwa akipitia.

•Aliweka wazi kuwa msongo wa mawazo ambao ulimuathiri ulitoka kwa mitandao ya kijamii na sio athari za baada ya kujifungua.

Carol Muthoni katika studio za Radio Jambo
Carol Muthoni katika studio za Radio Jambo
Image: RADIO JAMBO

Muigizaji mashuhuri wa Kenya Caroline Muthoni almaarufu Carrol Sonie amesisitiza kwamba alichukua mapumziko kutoka kwa kuunda maudhui kwenye mitandao ya kijamii kutokana na masuala ya kisaikolojia aliyokuwa akipitia.

Katika mahojiano na Obinna TV, mrembo huyo mwenye umri wa miaka 25 alifichua kuwa mambo aliyokuwa akipitia kufuatia kutengana na mchekeshaji Mulamwah yalimuathiri sana hadi akakaribia kurukwa na akili.

Sonie alisema ni vipindi vya ushauri nasaha vilivyofadhiliwa na mchekeshaji Nasra Yusuf ambavyo vilivyomuokoa na kumfanya arudi katika hali nzuri ya kiakili.

"Nilichukua mapumziko na kufanya matibabu ya ushauri nasaha. Nilipitia matibabu , ilinibidi kwa sababu nilikuwa nikiipoteza. Ushauri ulinifanya nielewe na kujua ni kwa nini nilikuwa nikipitia yale ninayopitia. Ndiyo maana nilipumzika,” Carrol Sonie alisema.

Aliongeza, “Kwa kweli, Nasra ni yeye alinisaidia. Nilikuwa nachizi, nilikuwa naamka napata nimetrend sijui nimefanya nini nashangaa nimedo? Hiyo yote ilikuwa ikiathiri kiakili na sikujua niende wapi ama kwa nani. Namshukuru Nasra, alinisaidia, alinilipia matibabu, nilienda kwa miezi mitatu. Yeye (Nasra) alikuwa ananiamsha kila asubuhi niende therapy.”

Mama huyo wa binti mmoja aliweka wazi kuwa msongo wa mawazo ambao ulimuathiri ulitoka kwa mitandao ya kijamii na sio athari za baada ya kujifungua.

“Msongo wangu wa mawazo ulitokana na unyanyasaji wa mtandaoni na kutokana na kudhalilishwa. Iliniingia kichwani, iliathiri sana afya yangu ya akili,” alisema.

Sonie alibainisha kuwa kabla ya kwenda kwa matibabu, hakujua jinsi ya kushughulikia chuki kwenye mitandao ya kijamii, jambo ambalo ameweza kufanya sasa.

"Kwa sasa ninachukulia kila kitu kuwa kizuri, kiwe kizuri au kibaya. Maoni na unachosema kunihusu haijalishi,” alisema.

Aidha, mpenzi huyo wa zamani wa Mulamwah alisema kuwa wazazi wake pia waliathiriwa na chuki aliyokuwa akipokea kwenye mitandao ya kijamii, lakini walimsaidia kushughulikia mambo.